Dk. Mukwege wa Congo atunukiwa Tuzo Mbadala ya Nobel
2 Desemba 2013Dakta Mukwege mkurugenzi wa Hospitali ya Panzi ilioko kwenye mji wa mashariki wa Congo wa Bukavu leo anatunukiwa Tuzo hiyo ya Haki ya Kuishi ambayo inajulikana zaidi kama ni tuzo ya mbadala ya Nobel mjini Stockholm kutokana na juhudi zake za kuwatibu wanawake ambao ni wahanga wa ubakaji.
Daktari huyo ambaye hasa anashughulikia upasuaji wa magonjwa ya wanawake mara kwa mara amekuwa akikemea ukatili wa ngono dhidi ya wanawake ambao umekuwa ukitumika kama silaha ya vita.
Tangazo la kutunukiwa kwa tuzo hiyo lilitolewa mwezi wa Septemba na Wakfu wa Haki ya Kuishi limeamsha furaha katika nchi alikozaliwa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Therese Mema wa Tume ya Haki na Amani ya Dayosisi ya Bukavu amesema Mukwege amekuwa msaada mkubwa kwa wanawake kwa kuwatetea na kuwashauri katika fani zote lakini wakati huo huo ni mnyenyekevu na ndio maana wamefarajika sana kwa dunia kumpa tuzo hiyo.
Kilichoshaijiisha kazi yake
Hayo ndio maisha yake ya kikazi daktari huyo mwenye umri wa miaka 58. Mukwege anasema chanzo cha shajiisho ni baba yake ambaye ni mchungaji aliembariki kuwasaidia watu wengine.
Kwa Tuzo ya Olof Palme aliyotunukiwa mwaka 2009 anasema kwake yeye hicho ni kitu kidogo sana lakini alijiambia mwenyewe kwamba itakuwa vyema kuendelea na kazi hiyo ya kuwasaidia watu. Baada ya kusomea udaktari katika nchi jirani ya Burundi alifanya kazi katika hospitali ya mji mdogo wa Lemera katika eneo la vijijini Kivu ya Kusini.
Alifadhaishwa na idadi ya wanawake wanaokufa kila siku katika kijiji hicho kwa sababu za uzazi.Hilo ndilo lililomchochea asomee zaidi matibabu ya wanawake ambapo alikwenda Ufaransa kusomea juu ya magonjwa ya kike na ukunga.
Aliporudi tena Congo baada ya masomo yake wakati huo ikiitwa Zaire Mukwege alikuja kukabiliwa na changamoto mpya ambapo katika miaka ya 1990 Lemera ilikuwa katikati ya kanda ya vita vya Congo na iliharibiwa kabisa hapo mwaka 1996 ambapo makundi mbali mbali ya wapiganaji yalitumia ubakaji kama silaha ya vita.
Kwa msaada wa kimataifa Dakta Mukwege alianzisha mradi mpya ambayo ni hospitali ya Panzi katika mji mkuu wa jimbo wa Bukavu ambapo kutokana na idara yake ya magonjwa ya kike hospitali hiyo ikajipatia umashuhuri kwa haraka sana.
Katika hospitali hiyo Mukwege kwa kushirikiana na wenzake wamekuwa wakiwasaidia wanawake na wasichana ambao wamekumbwa na visa vya ubakaji kutoka makundi yanayopingana vijijini. Mbali na kuwa daktari Mukwege kwa muda mrefu amekuwa akitetea haki za binaadamu nchini Congo.
Ameanzisha mipango ya msaada wa kisaikolojia na wa kisheria kwa wahanga wa ubakaji.Mukwege anataka kushughulikia mzizi wa tatizo hilo na kukemea vita vya kiuchumi vinavyoshamiri nchini Congo ambapo waasi na serikali wanagombania udhibiti wa mapato ya mali asili.
Ajizatiti kwa amani na haki
Habari za kutunukiwa kwa tuzo yake hiyo mpya pia zilimfurahisha mshirika wake Gisela Schneider mkurugenzi wa Taasisi ya Shughuli za Matibabu ya Ujerumani (Difäm) ambayo kwa miaka 10 taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Mukwege na kusadia hospitali yake hiyo pamoja na kutowa mafunzo.
Schneider ambaye amemtembelea Mukwege huko Congo wiki nne zilizopita kabla ya kutangazwa kutunukiwa kwa tuzo hiyo amekaririwa akisema " Huu ni uamuzi mzuri kabisa kwani mtu anayetunukiwa hapo amejizatiti kwa dhati katika maisha yake yote kwa ajili ya kutumikia amani na haki.
Mwezi wa Oktoba mwaka jana Mukwege alisunurika chupu chupu kuuwawa baada ya watu wenye silaha kuivamia nyumba yake huko Bukavu na alilazimikia kukimbilia Ubelgiji kabla ya kurudi tena katika hospitali yake ya Panzi hapo mwezi wa Januari mwaka huu. Pamoja na washindi wengine watatu Mukwege atapokea euro 230,000.
Mwandishi: Philipp Sandner/Mohamed Dahman
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman