1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund kuharibu karamu ya Tuchel mjini Munich?

31 Machi 2023

Borussia Dortmund inaweza kuivamia na kuchafua hafla ya kumtambulisha kocha mpya wa Bayern Munich ambaye ni kocha wao wa zamani Thomas Tuchel Jumamosi

https://p.dw.com/p/4PYfZ
Thomas Tuchel | neuer Trainer bei Bayern München
Picha: Sven Hoppe/picture alliance/dpa

Borussia Dortmund inaweza kuivamia na kuchafua hafla ya kumtambulisha kocha mpya wa Bayern Munich ambaye ni kocha wao wa zamani Thomas Tuchel Jumamosi na kupiga hatua nyingine kukaribia kuzuia jaribio la miamba hao kubeba taji la Bundesliga kwa mara ya 11 mfululizo.

Dortmund wako kileleni mwa msimamo na pengo la pointi moja dhidi ya Bayern lakini watavaana na mahasimu wao hao wa kinyang'anyiro cha taji katika dimba la Allianz Arena, ambalo limekuwa eneo la makaburi kwa malengo yao katika enzi ya baada ya kocha Jurgen Klopp.

Thomas Tuchel
Tuchel alikuwa Dortmund kuanzia 2015-2017Picha: picture alliance / Arne Dedert/dpa

Wakiwa wameshinda 9 kati ya mechi 10 za ligi katika mwaka wa 2023, Dortmumd wanaingia katika mechi hii wakiwa katika fomu nzuri kabisa.

Bayern wameshinda tano kati ya 10 katika kipindi hicho, kuelekea kutimuliwa wiki iliyopita kwa meneja Julian Nagelsmann na kumpa majukumu kocha wa zamani wa BVB Tuchel.

Ushindi wa Dortmund wa mechi ya ligi mjini Munich ulikuja mwaka wa 2014 chini ya Klopp wakati ambapo mbio za taji zilikuwa tayari zimeshaamuliwa katika upande wa Bayern. Tangu wakati huo, Bayern wameshinda mechi nane za ‘Der Klassiker‘ mfululizo, na kufunga mabao 33 na kufungwa sita pekee.

"Ni mechi kubwa sana kwetu sote. Ni suala la kujenga imani na matarajio”, amesema Tuchel. "Hakuna changamoto kubwa kuliko kuanza Maisha yangu hap ana mechi dhidi ya Dortmund. Ni mtanange mkubwa kabisa katika kandanda la Ujerumani, na ina utaamu fulani ukizingatia hali ya sasa ya msimamo wa ligi."

Matokeo ya sare yataibakisha Dortmund kileleni na pengo la pointi moja huku kukisalia na mechi nane msimu kukamilika. Hata hivyo kiungo Emre Can anasema "tunakwenda kule kushinda. Itakuwa kazi ngumu sana, lakini tunajiamini."

Kocha wa Dortmund Edin Terzic amesema uteuzi wa Tuchel umeilazimu timu yake kubadili maandalizi ya mchuano huu. "Hatujui ni kiasi gani Tuchel ataendeleza kile alichokifanya Julian Nagelsmanna katika wiki chache zilizopita, au kama ataleta mawazo mapya kabisa. Lakini kile ambacho hakijabadilika ni kuwa bado wana kocha bora zaidi kwenye benchi na timu bora uwanjani."

AFP