De Mistura: Usitishaji mapigano Syria waheshimiwa
4 Machi 2016De Mistura alisisitiza kwamba mpaka sasa kuna ufanisi, siku sita tangu makubaliano ya kusitisha uhasama yalipoanza kutekelezwa, akisema kiwango cha machafuko kimepungua. Katika siku tano zilizopita, jumla ya watu 73 wameuliwa kote nchini Syria, kwa mujibu wa shirika linalofuatilia masuala ya haki za binaadamu la Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuongoza mkutano wa kundi la kimataifa linalosaidia kuusuluhisha mzozo wa Syria, katika afisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, De Mistura pia alisema hali inabakia kuwa ya wasiwasi kwa kuwa kuna mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea katika maeneo ya mji mkuu Damascus, Latakia na Homs.
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano na kuongeza juhudi za kupeleka misaada Syira, hususan kwa watu karibu nusu milioni katika maeneo yaliyozingirwa.
"Msaada wa kibinaadamu na usitishaji mapigano ni muhimu sana katika kujenga mazingira mazuri na uaminifu. Lakini hakuna masharti yoyote; masharti ni kwa kila mtu kuona kwamba kuna mchakato wa kisiasa na suluhisho la kisiasa litashughulikia janga la Syria," alisema De Mistura.
De Mistura alisema mazungumzo kuhusu mzozo wa Syria yataanza tena Jumatano wiki ijayo, ingawa wajumbe watawasili baadaye kutokana na sababu za uratibu.
Juhudi zaidi zifanyike
Ufaransa na Uingereza zilisema jitihada zaidi zinahitajika kutuliza hali ya mambo nchini Syria. Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron alisema atazungumza na rais wa Urusi Vladimir Putin kumhimiza asitishe mashambulizi Syria.
Cameron alisema, "Urusi inahitaji kukomesha mashambulizi yake dhidi ya raia wa Syria na upinzani wenye msimamo wa wastani na ikubali kuwa panahitajika kipindi cha mpito kuondokana na rais Assad na kuelekea kwa kiongozi mpya atakayeiunganisha Syria na kuleta amani na uthabiti nchini humo."
Cameron aidha alisema rais wa Ufaransa Francois Hollande na kansela wa Ujerumani Angela Merkel, pia watashiriki katika mazungumzo hayo na rais Putin leo, kwa lengo la kuratibu njia za kupata ufanisi katika mazungumzo yatakayofanyika mjini Geneva wiki ijayo. Merkel na Hollande watakutana leo mjini Paris, Ufaransa.
Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza wanakutana pia mjini Paris kujadili maendeleo yaliyopatika katika kutekeleza usitishaji uhasama nchini Syria na juhudi za kimataifa kupeleka misaada nchini humo.
Mwandishi:Josephat Charo
Mhariri: Yusuf Saumu