Dani Alves ahukumiwa miaka 4.5 jela kwa ubakaji
22 Februari 2024Mahakama ya Uhispania imemuhukumu mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Brazil Dani Alves kifungo cha miaka minne na nusu jela baada ya kumkuta na hatia ya kumbaka mwanamke katika klabu ya Barcelona mnamo Desemba 2022.
Pia ilimuamuru mshindi huyo mara tatu wa Ligi ya Mabingwa kuwekwa chini ya uangalizi kwa miaka mitano baada ya kutumikia kifungo chake jela, na kumtaka alipe euro 150,000, sawa na dola 162,000 kama fidia kwa mwathiriwa.
Mahakama hiyo pia imempiga marufuku Alves kumkaribia mwathiriwa nyumbani au mahali pa kazi na kutokuwa na mawasiliano naye kwa njia yoyote kwa miaka tisa.
"Mwathiriwa hakuridhia na kuna ushahidi kwamba, zaidi ya ushuhuda wa mlalamikaji, unaruhusu ubakaji kuzingatiwa kuwa umethibitishwa," mahakama ya Barcelona iliandika katika taarifa.
"Mahakama inazingatia kama jambo lililothibitishwa, ukweli kwamba mshtakiwa alimshika mlalamikaji ghafla, akamuangusha chini na kumuingilia ukeni, na kumzuia asisogee, huku mlalamikaji akisema hapana na alitaka kuondoka."
Waendesha mashtaka walikuwa wamependekeza kifungo cha miaka tisa jela kwa Alves mwenye umri wa miaka 40 na uangalizi wa miaka kumi.
Alves, ambaye alitoa ushahidi katika kesi yake kwamba alifanya mapenzi na mwanamke huyo kwa makubaliano, anaweza kukata rufaa.
Mmoja wa wanasoka mahiri duniani aliyezichezea Barcelona na Paris Saint-Germain katika maisha yake ya soka, Alves alifikishwa mahakamani mapema mwezi huu kwa tuhuma za kumbaka mwanamke katika klabu ya Sutton mapema Disemba 31, 2022.
Mlalamikaji ambaye alitoa ushahidi nyuma ya skrini ili kulinda utambulisho wake -- alisema Alves alimlazimisha kufanya ngono katika choo cha faragha cha kilabu hiyo licha ya kumwomba amwachie, na kusababisha "uchungu na hofu", kulingana na waendesha mashtaka.
Rafiki aliyekuwa naye aliangua kilio alipokuwa akiiambia mahakama jinsi mwathiriwa alivyokuwa "akilia bila kujizuia" baada ya kutoka bafuni, akisema Alves "amemuumiza sana".
Maafisa wa polisi waliomuhudumia mwanamke huyo walielezea mahakama kuhusu hali ya mwathiriwa ya kufadhaika na "mshtuko" walipofika kwenye klabu hiyo, pamoja na wasiwasi wake kwamba "hakuna mtu angemwamini" ikiwa angewasilisha malalamiko.
Alves, ambaye alikuwepo mahakamani katika kipindi chote cha kesi yake ya siku tatu, alieleza kuwa kujamiiana kwake na mwanamke huyo kulikuwa kwa makubaliano na alikana kumpiga na kumvuta nywele.
"Mimi sio mwanaume wa aina hiyo, siyo mkatili," aliiambia mahakama baada ya wakili wake wa utetezi kuuliza ikiwa alimlazimisha kufanya ngono.
"Iwapo alitaka kuondoka, angeweza kuondoka, hakuwa na wajibu wa kuwa hapo," aliongeza.
Soma pia: Dani Alves "autafuna" ubaguzi wa rangi
Ushawishi wa pombe
Rafiki wa Alves ambaye alikuwa naye usiku huo alitoa ushahidi kwamba mchezaji huyo wa kandanda alikunywa mvinyo na pombe kali kabla ya kwenda kwenye klabu hiyo.
Mkewe Joana Sanz mwenye umri wa miaka 31 aliambia mahakama Jumanne kwamba alionekana kulewa sana aliporudi nyumbani kwao Barcelona usiku huo na hakutaka kuzungumza naye kwa sababu ya "hali aliyokuwa nayo".
Wakili wa Alves, Inés Guardiola, amesema atakata rufaa.
David Sáenz, mwanachama wa timu ya wanasheria wa mwathiriwa, alisema, "tumeridhika, kwa sababu uamuzi huu unatambua kile ambacho tumekuwa tukijua siku zote, kwamba mwathiriwa alisema ukweli na kwamba aliteseka."
Alves, ambaye anatoka katika familia maskini huko Juazeiro katika Jimbo la Bahia nchini Brazil, awali alikana kumfahamu mwanamke huyo katika mahojiano ya televisheni lakini baadaye alikiri kufanya naye mapenzi, akisema ni maelewano. Aliliambia gazeti la La Vanguardia mnamo Juni kwamba alidanganya kwa sababu aliogopa mkewe angemwacha.
Mchezaji huyo amekuwa kizuizini tangu alipokamatwa mjini Barcelona mnamo Januari 2023. Maombi yake ya kuachiliwa kwa dhamana yamekataliwa mara kwa mara na mahakama ambazo zilimwona kuwa na hatari ya kukimbia kwa sababu ya utajiri wake.
Brazil haiwasafirishi raia wake amabo wamehukumiwa katika nchi nyengine.
Alves anazingatiwa kama mmoja wa mabeki bora zaidi wa wakati wote, akishinda vikombe 42 wakati wa kazi yake iliyompa mafanikio makubwa.
Kilele cha maisha yake ya soka kilikuwa Barcelona kati ya 2008 na 2016 aliposhinda mataji 23. Wakati wa kukamatwa kwake, alikuwa amepewa mkataba na klabu ya Mexico ya Pumas UNAM lakini alitimuliwa mara baada ya kukamatwa.