Damu yazidi kumwagika Pakistan
16 Oktoba 2009Watu wasiopungua 12 wameuwawa leo kufuatia shambulio dhidi ya kituo cha polisi huko Peshawar, kaskazini magharibi ya Pakistan. Huu ni mfululizo wa mashambulio ya kikatili ambayo kwa sehemu kubwa Wataliban wanasema wanabeba dhamana.
Duru za hospitali zinazungumzia juu ya wahanga 12. Askari polisi watatu ni miongoni mwao. Afisa wa ngazi ya juu wa polisi alisema hapo awali mwanammke mmoja na mwanawe ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha yao.
Shambulio la leo ni la sita mnamo muda wa siku 12, ikiwa ni pamoja na milolongo 2 ya mashambulio dhidi ya makao makuu ya jeshi karibu na mji mkuu, Islamabad, na dhidi ya vituo vitatu vya polisi huko Lahore-mashariki ya Pakistan. Mlolongo huo wa mashambulio ambayo Wataliban wamedai kubeba dhamana ya mengi kati yao yamegharimu maisha ya watu wasiopungua 176.
"Mtu aliyeyatolea mhanga maisha yake alijiripua pamoja na gari yake karibu na jengo la idara ya upelelezi- CIA katika mtaa wa kijeshi wa mji wa Peshawar, mji mkuu wa jimbo la kaskazini magharibi lenye wakaazi zaidi ya milioni mbili na nusu-"amesema afisa wa kikosi cha polisi chenye kutegua miripuko-Shafqat Malik.
"Tumehesabu maiti 11 na majeruhi 13 hospitali" amesema kwa upande wake afisa wa polisi ya Peshawar Mohammed Gul, alipohojiwa na shirika la habari la Ufaransa AFP.
Vituo vya televisheni vimeonyesha jumba kubwa la matofali mekundu lililoporomoka lote huku magari ya kusafirisha wagonjwa yakisheheni askari polisi na wanajeshi waliojeruhiwa. Msikiti uliokua karibu na hapo nao pia umehujumiwa.
Jana, waasi wasiopungua 11 waliokua na bunduki za rashasha, maguruneti na kuvalia vizibao viliovyosheheni miripuko walivamia takriban kwa wakati mmoja makao makuu ya idara ya upelelezi, chuo kikuu cha polisi na kituo cha mazowezi ya vikosi maalum vya polisi mjini Lahore. Askari polisi mmoja anasema:
Tumegundua kizibao kilichosheheni miripuko na maguruneti.Mlangoni kuna maiti mbili na polisi wasiopungua wawili hawajulikani waliko."
Hakuna aliyedai kuhusika na mashambulio hayo lakini yanaonyesha ni mlolongo wa mashambulio ya Wataliban wanaojiripua yaliyoanza zaidi ya miaka miwili iliyopita na kugharimu maisha ya watu wasiopungua 2300 nchini Pakistan.
Wimbi hili la mashambulio limezidi kupata nguvu siku za hivi karibuni na kugharimu maisha ya watu wasiopungua 176.
Kundi la Wataliban wa Pakistan-TTP,limedai kuhusika na baadhi ya mashambulio hayo.
Hivi karibuni Wataliban waliapa kuwa watalipiza kisasi kwa kuuliwa muasisi wa kundi lao,Baitullah Mehsud, Agosti tano iliyopita.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri:Othman Miraji