1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cyril Ramaphosa ndiye rais mpya wa ANC

Sylvia Mwehozi
19 Desemba 2017

Makamu wa rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amechaguliwa kuwa rais wa chama tawala cha African National Congress ANC, katika uchaguzi uliokuwa na ushindani na utakaoamua mwelekeo wa nchi hiyo na chama .

https://p.dw.com/p/2pcNY
Südafrika Cyril Ramaphosa, neuer Präsident ANC
Picha: Reuters/S. Sibeko

Kama kiongozi wa ANC, Ramaphosa mwenye umri wa miaka 65, ambaye amewahi kuwa kiongozi wa shirikisho la biashara na mfanyabiashara mkubwa na ambaye hivi sasa ni miongoni mwa matajiri wakubwa wa Afrika Kusini, ana uwezekano wa kuwa rais ajaye wa Afrika Kusini pale uchaguzi mkuu utakapofanyika mwaka 2019.

Ameahidi kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi, ujumbe ambao umepongezwa na wawekezaji wa kigeni. Rais Jacob Zuma aliyeandamwa na rushwa pamoja na kashfa, ameharibu taswira ya ANC ndani na nje ya nchi. Chama hicho ambacho wakati mmoja kiliwahi kuongozwa na Nelson Mandela, kiko katika mgawanyiko mkubwa kwa hivi sasa.

Südafrika ANC Parteitag Zuma und Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma katika mkutano wa chama Picha: Getty Images/AFP/M. Safodien

Ramaphosa alipata ushindi mdogo dhidi ya Nkosazana Dlamini-Zuma mwenye miaka 68, waziri wa zamani na mtalaka wa Jacob Zuma katika kura ya Jumatatu na kuashiria wakati muhimu kwa ANC, ambayo ilianzisha utawala wa waafrika walio wengi chini ya uongozi wa Mandela miaka 23 iliyopita. Bontle Mpakanyane ni Afisa wa tume ya uchaguzi ya Afrika Kusini aliyetangaza matokeo hayo. "Na mgawanyo wa kura uko hivi, comrade Nkosazana Dlamini-Zuma amepata kura 2261 na Comrade Cyril Ramaphosa amejipatia kura 2440. Tunamtangaza comrade Cyril Ramaphosa kuwa rais mpya wa chama cha Africa National Congress."

Wachambuzi wanasema uchungu wa kuwania madaraka baina ya Ramaphosa na Dlamini-Zuma umeongeza mwanya kwamba chama kitajikuta katika wakati mgumu kuunda sera na kinaweza kugawanyika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2019. Baada ya uchaguzi huu, Ramaphosa anakuwa ndiye mpeperusha bendera katika uchaguzi mkuu, lakini atapaswa kushindana na washirika wa Dlamini-Zuma katika uongozi wake, ikimaanisha kuwa sera zao zitakuwa tofauti.

Südafrika ANC Parteitag Ramaphosa und Nkosazana Dlamini-Zuma
Ramaphosa na Nkosazana Dlamini-Zuma Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Hadebe

Kwa wafuasi wake, mafanikio ya kibiashara ya Ramaphosa yanamfanya kuwa mtu anayefaa katika nafasi ya kuubadilisha uchumi na kupunguza asilimia 28 ya ukosefu wa ajira na kushuka kwa viwango vya ukopaji.

Baadhi ya wachambuzi wanaona kwamba Ramaphosa atakabiliwa na kibarua kigumu kisiasa, ikiwa Zuma ataendelea kuwa rais. Ingawa Zuma aliachia ngazi kama kiongozi wa chama katika mkutano mkuu lakini muhula wake wa urais unamalizika mwaka 2019 wakati uchaguzi utakapofanyika. Zuma amekabiliwa na madai ya rushwa tangua aingie madarakani 2009 lakini wakati wote amekana madai hayo. Rais huyo pia amekabiliwa na madai kwamba rafiki yake, mfanyabiahsara maarufu Gupta, amekuwa na ushawishi katika serikali yake. Wote kwa pamoja wamekana tuhuma zozote. Zuma pia ameepuka mara kadhaa kura ya kutokuwa na imani naye bungeni juu ya utendaji wake kama mkuu wa nchi.

Kiongozi huyo wa ANC anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza kesho Jumatano wakati mkutano mkuu wa chama utakapokuwa ukimalizika.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga