CSU kuzidi kumbana Merkel juu ya wahamiaji
18 Juni 2018Miaka mitatu baada ya uamuzi wake wa kuwaruhusu wahamiaji wanaokimbia vita nchini Syria na Iraq kuingia nchini mwake, bado Kansela Merkel anahangaika kuyapatia malalamiko ya washirika wake wa Bavaria, chama cha CSU, majibu yanayotosha kuhusiana na sera yake ya wakimbizi.
Na Jumatatu ya leo, linasema gazeti mashuhuri la hapa Ujerumani, Bild, kwamba ni "siku yenye mashaka kwa Angela Merkel na kwa serikali yake."
Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria, Markus Söder, anasema kuwa Ujerumani haipaswi kufanya makosa yaliyofanywa na mataifa mengine ya Ulaya ambayo sasa yanatawaliwa na serikali zinazotokana na vyama vya siasa kali au vinavyotumia hamasa za umma kujikusanyia kura.
"Ikiwa tutafanya makosa kwamba sisi, kama mataifa mengine ya Ulaya, hatuwezi kufanya maamuzi kama vyama vya kiraia, hatimaye wanasiasa wanaotumia hamasa za umma tu ndio watakaokuwa na nafasi. Nami sitaki wao wawe watetezi pekee wa raia, nataka sisi ndio tuwe na nafasi hiyo," aliongeza Söder.
Ulaya yapasuka tena kuhusu wahamiaji
Katika siku za hivi karibuni, mataifa ya Umoja wa Ulaya yamejikuta yakiingia tena kwenye migogoro kutokana na suala la wahamiaji, baada ya Itali kukataa kuiruhusu meli ya uokozi iliyobeba wahamiaji 630 kutia nanga kwenye bandari zake.
Malta pia ilikataa kuipokea meli hiyo, hali iliyochochea mashambulizi makali ya maneno kutoka Umoja wa Ulaya, hadi pale Uhispania ilipokubali kuwachukuwa wakimbizi hao.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani na anayetokea chama cha CSU cha Bavaria, Horst Seehofer, amekuwa akiukosoa vikali msimamo wa kiliberali wa Kansela Merkel kwenye suala hili la wahaimiaji, ambao anasema umewawezesha waomba hifadhi milioni moja kusajiliwa nchini Ujerumani tangu mwaka 2015.
Seehofer anataka wahamiaji walioingia Ulaya kupitia nchi nyengine wasiruhusiwe kuomba hifadhi nchini Ujerumani, na badala yake warejeshwe kwenye mataifa hayo, mara nyingi yakiwa ni Italia au Ugiriki. Lakini Kansela Merkel anahoji kwamba uamuzi huo utayafanya mataifa ya kusini mwa Ulaya pekee kubeba mzigo wa wakimbizi.
"Hili ni changamoto linalohitaji jawabu la Ulaya. Na nadhani hili ni moja ya maswala muhimu sana kwa uthabiti wa Ulaya," alisema kwenye ujumbe wake kwa njia ya vidio.
Hadi muda tunaenda hewani, maafisa wa ngazi za juu wa vyama cha CDU na CSU wanakutaka katika vikao tafauti mjini Berlin na Munich kuzungumzia suala hili. Viongozi wa pande zote mbili wanatazamiwa kuzungumza na waandishi wa habari baadaye leo.
Kabla ya vikao hivyo, katibu mkuu wa CSU, Markus Blume, alisema mpango wa Seehofer kuhusu wahamiaji ulikuwa na baraka zote za chama chao.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman