Croatia na Argentina zatinga nusu fainali ya Kombe la Dunia
10 Desemba 2022Argentina imefanikiwa kusonga mbele kwenda hatua ya robo fainali baada ya mchezo wa kukata na shoka dhidi ya Croatia uliolazimisha mshindi baina ya timu hizo mbili kupatikana kwa mikwaju ya penati.
Argentina iliilaza Uholanzi kwa peneti 4-3 baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika kwa bao 2-2 na nyingine 30 za nyongeza kufikia mwisho bila timu yoyote kutikiza nyavu za mwengine.
Mlinda mlango wa Argentina Emiliano Martinez alipangua mikwaju miwili ya mwanzo ya peneti za wachezaji wa Uholanzi huku kiungo wa miamba hiyo ya soka ya Amerika ya Kusini Lautaro Martinez alitikisa nyavu kwa mkwaju wa mwisho wa penati uliofungua milango ya Argentina kufuzu hatua ya nusu fainali.
Mchezo huo ulifikia hatua ya mikwaju ya penati kwa mbinde. Hadi dakika saba kabla ya kumalizika kwa dakika 90, Argentina ilikuwa ikiongoza kwa 2-0. Hata hivyo Uholanzi iliwashangaza mashabiki wa soka kwa kupachika wavuni magoli mawili ya kusawazisha kabla ya kipenga cha mwamuzi kupulizwa.
Messi aipatia Argentina bao la pili lakini Uholanzi yasawazisha kimaajabu
Goli la kwanza la Argentina lilifungwa mnamo dakika ya 35 na mshambuliaji Nahuel Molina na baadaye Lionel Messi aliipatia timu yake bao la pili kwa mkwaju wa penati baada ya walinda mlango wa Uholanzi kutenda madhambi ndani ya 18.
Mabadiliko yaliyofanywa na Uholanzi na kumwingiza mshambuliaji Wout Weghorst yalisadifu kuwa na manufaa. Mchezaji huyo ndiye aliipatia timu hiyo mabao yote mawili ikiwemo lile la sekunde za mwisho kabisa kabla ya kumalizika kwa dakika 10 zilizoongezwa baada ya dakika 90.
Mchezo huo wa jana usiku ulitawaliwa pia na kadi nyingi za njano. Mwamuzi Antonio Mateu kutoka Uhispania aliinua mkono mara 16 kuonesha kadi ya njano ikiwemo kwa Lionel Messi.
Brazil ya Neymar yalambishwa shubiri na vijana wa Croatia
Wakati Argentina inasonga mbele, miamba mingine ya soka ya America ya Kusini, timu ya taifa ya Brazil imeoneshwa mlango wa kutokea kwenye michuano hiyo ya Kombe la Dunia baada ya kupoteza mechi ya kwanza ya robo fainali dhidi ya Croatia.
Mechi hiyo iliyochezwa jioni kwa saa za Afrika Mashariki pia iliamuliwa kwa mikwaju ya penati. Croatia ilipata ushindi wa penati 4-2 na kujiwekea nafasi kwenye hatua ya nusu fainali kwa mara ya pili mfululizo kwenye Kombe la Dunia, mara hii watapambana na Argentina.
Nyota wa timu ya Brazil Neymar alimwaga machozi baada ya mchezo, uliozima ndoto za timu yake kurejea na kikombe nyumbani. Hii leo michezo mingine miwili ya robo fainail itapigwa.
Morocco inayobeba matumaini ya bara la Afrika ina miadi na Ureno wakati England itapambana Ufaransa kuamia nani atasonga mbele na timu gani itakusanya virago.