1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COVID-19 na Brexit kujadiliwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya

15 Oktoba 2020

Kuongezeka kwa visa vya COVID-19 Ulaya kumezusha mjadala Brussels. Ni jinsi gani hatua za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona na madhara yake katika uchumi vinaweza kuepukwa? Na tatizo hili bado halijatatuliwa.

https://p.dw.com/p/3jy3B
Symbolbild EU Corona
Picha: Yves Herman/Reuters

''Tunakutana katika mazingira magumu, kwa sababu ya maambukizi ya COVID-19 yanaongezeka na uhusiano na Uingereza ukiwa katika ajenda''.

Kwa kauli hio isiyokuwa na matumani ndiyo anavyoanza kuandika barua yake Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel kuwaalika viongozi wa nchi 27 wanachama ambao wanakutana leo na kesho Ijumaa mjini Brussels.

Janga la virusi vya corona na mzozo wa muda mrefu kuhusu makubaliano na Uingereza ambayo imejiondoka katika Umoja wa Ulaya ndiyo yataongoza majadiliano.

Katika kupambana na janga hilo, ambapo wimbi la pili limeanza barani Ulaya, kila nchi inategemea kuchukua hatua tofauti. Ufaransa, kama ilivyo kwa Uholanzi na Italia imetangaza vizuizi vipya katika mikusanyiko binafsi na kwenye mikahawa.

Brüssel EU Sondergipfel Charles Michel
Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel Picha: Dursun Aydemir/AA/picture-alliance

Jamhuri ya Czech itaingia katika awamu ya pili ya kuzifunga shughuli za umma kutokana na visa vya maambukizi kuongezeka kwa kasi. Nchini Ujerumani kuna mjadala mkali kuhusu vizuizi vya ndani vya kusafiri kati ya majimbo ya shirikisho.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliwaambia viongozi wa mikoa na mameya wa Ulaya mjini Brussels kwa njia ya vidio, kwamba anafuatilia ongezeko la maambukizo katika maeneo mengi ya Ulaya kwa wasiwasi mkubwa, na kuongeza kwamba hali bado ni mbaya.

Majadiliano magumu ya bajeti

Kansela Merkel ambaye ataendelea kuwa Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya hadi mwishoni mwa mwaka huu, analishinikiza Bunge la Ulaya kuidhinisha mfuko wa uokozi wa janga la corona na bajeti ya Umoja wa Ulaya kwa miaka saba ijayo ambayo ni takriban Euro bilioni 1.8 haraka iwezekanavyo. ''Lazima tuzipate pesa kwa wakati, ili mfuko huo uanze kutumika mwanzoni mwa mwaka 2021," alisema Merkel. 

Poland imeukataa mpango huo. Naibu Waziri Mkuu wa Poland Jaroslaw Kaczynski anatishia kutumia kura ya turufu katika mazungumzo ya bajeti. Umoja wa Ulaya umekuwa ukikosoa mageuzi ya mahakama Poland, ambayo yamekuwa yakidhoofisha utawala wa sheria nchini humo.

Corona-Gipfel  I  Merkel und Ministerpräsidenten
Kansela wa Ujerumani, Angela MerkelPicha: Stefanie Loos/AFP/dpa/picture-alliance

Katika suala la Brexit, wakuu wa nchi na serikali hawana cha kujadili, kwa sababu mwenzao, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson hata hajaalikwa. Mazungumzo kuhusu makubaliano ya kibiashara na Uingereza bado yamekwama.

Pande zote zinatupiana lawama kwa kutokubaliana kuhusu masuala tete kama vile msaada wa serikali, uvuvi na udhibiti wa sheria wa makubaliano yoyote.

Michel, amesema wakuu wa Umoja wa Ulaya wamesema wana nia ya kufikia makubaliano ya haki, lakini sio kwa gharama yoyote ile. Muda wa mwisho uliowekwa na Boris Johnson ambao unamalizika leo, huenda ukapuuzwa katika mkutano huo wa kilele wa Brussels. Johnson alitangaza kuwa atatoa tamko baada ya mkutano huo jinsi serikali yake itakavyoendelea kwa upande wake.

Viongozi hao wa Umoja wa Ulaya pia watajadiliana kuhusu malengo ya kulinda mabadiliko ya tabia nchi ya umoja huo. Hapa kuna utata wa kiasi gani cha gesi chafu inayoharibu mazingira kinapaswa kupunguzwa ifikapo mwaka 2030.

Katika siku ya pili ya mkutano huo wa kilele, mkakati wa Afrika na masuala kadhaa yenye utata kuhusu sera ya kigeni kuanzia Belarus hadi Uturuki yatakuwa kwenye ajenda.