Corona yaendelea kuwa pasua kichwa
28 Oktoba 2020Mambukizi ya virusi vya corona yameanza kuongezeka hususani wakati huu ambapo kipindi cha baridi kinawadia. Hapa nchini Ujerumani maambukizi yamefikia kiwango cha watu zaidi ya elfu 10 kwa siku, hivyo kupelekea kuanzishwa kwa vizingiti vipya.Leo Jumatano Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amefanya mkutano na viongozi wa majimbo yote ya Ujerumana na kusisitiza kwamba shughuli mbali mbali zisizo za lazima kama vile za michezo na zile za kustarehe zitafungwa. Pia idadi ya watu kuonana nayo itapunguzwa, hivyo kutatiza shughuli nyingi za Krismasi ya mwaka huu.
Katika nchi nyingine za barani Ulaya, idadi ya maambukizi nchini Ufaransa imefikia watu zaidi ya elfu 50 kwa siku. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema huenda akaongeza masaa ya kutotoka nje pamoja kufungwa kwa shughuli mbali mbali kuanzia wikiendi ijayo au katika maeneo yenye maambukizi mengi.
Kwa upande mwingine nchini Ubelgiji maambukizi yamezidi kuongezeka kupelekea huduma za hospitali kuzidiwa, huku maelfu ya watu nchini Italia wameshudiwa wakiandamana kupinga ufungwaji wa shughuli mbali mbali. Urusi nako sheria za kuhakikisha watu wanavaa barakoa katika sehemu zenye watu wengi na kwenye usafiri wa umma, zimeanza kutumika kuanzia leo Jumatano.
Nchini Marekani, ambapo kuna maambukizi ya maelfu kwa maelfu ya watu kwa siku, tayari takribani watu 225,000 wameshapoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa COVID 19. India nchi inayoshika nambari mbili kwa idada kubwa ya maambikizi inayofikia milioni 8, leo Jumatano mamilioni ya watu wamejitokeza kwenda kupiga kura katika uchaguzi unaoendelea katika jimbo la Bihar. Wapiga kura wameshudiwa wakiwa kwenye foleni za kupiga kura bila kuzingatia vizuizi vya kudhibiti corona kama vile uvaaji wa barakoa na kuhakikisha umbali baina ya mtu na mtu.
Vizingiti hivi vinavyowekwa maeneo mbali mbali vinategemewa kuleta athari za kiuchumi, lakini nchi nyingi zinaona ni bora kuchukua hatua hizo kuzuia maambuki kwani mpaka sasa dawa na chanjo dhidi ya corona bado hazijahakikiwa.