1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Watu waliokufa kwa COVID -19 wapindukia 400,000

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
7 Juni 2020

Wakati huo huo serikali ya Brazil imesema imesimamisha zoezi la kuchapisha idadi ya watu waliokufa kwa COVID -19 au waliopata maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

https://p.dw.com/p/3dOo0
Brasilien Brasilia Präsident Jair Bolsonaro bei Pro-Regierungs Demonstration
Picha: Getty Images/A. Anholete

Hatua hiyo inakwenda kinyume na mapendekezo ya shirika la afya duniani WHO. Nchi hiyo kwa sasa ndio ina idadi kubwa ya vifo na maambukizi ya virusi vya corona katika nchi za Amerika ya Kusini.

Wakati huo huo madereva wa malori ambao ni miongoni mwa watoa huduma muhimu barani Afrika wanasema wanakabiliwa na unyanyapaa tangu kuzuka janga la maambukizi ya virusi vya corona. Kundi la watu hawa husafirisha bidhaa kama chakula, mafuta, vifaa na mahitaji mengine muhimu wakati mwingine wanapitia kwenye barabara zenye hatari hasa wakati huu ambapo ulimwengu unakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi. Madereva wa malori barani Afrika wanalalamika kuwa wao ndio wanatuhumiwa kwa kusambaza maambukizi ya virusi vya corona.

Ni kweli mamia ya madereva hao wa malori wameambukizwa virusi hivyo katika wiki za hivi karibuni,wanatoa malalamiko yao kwamba wananyanyaswa na kuchukuliwa kama wahalifu na mara nyingine wakamatwa na maafisa wa serikali hali amabyo inasababisha adha kwenye usafirishaji wa mizigo na kufanya shughuli za barabarani ziende polepole kutokana na  misongamano ya magari hayo ya kubeba mizigo.

Hali hiyo imeibua changamoto kwa serikali nyingi kwenye nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo mipaka mingi bado imefungwa kutokana na janga la corona, nchi hizo pia zinapambana juu ya jinsi ya kuyadhibiti maambukizi na kuendelea kwa shughuli za biashara. Nchi za Afrika mashariki zinajitahidi kufikia makubaliano ya pamoja.

Mamlaka za afya katika nchi za Afrika Mashariki bado hazina vifaa vya kutosha vya kupimia watu na hivyo basi zinategemea simu yz rununu za madereva wa malori kama njia moja wapo ya kuwafuatilia.

Malori yakiwa eneo la mpakani
Malori yakiwa eneo la mpakani Picha: Imago/Agencia EFE

Pontiano Kaleebu, anayeongoza Taasisi ya Utafiti wa Virusi nchini Uganda amesema kuweka mkazo na kufuatilia kwa karibu maeneo yanayodhaniwa kuwa na maambukizi ya kiwango kikubwa sio hatua za kibaguzi hata kidogo bali ni kutokana na hali halisi ilivyo.

Kwa upande wake  Aggrey Keya mtaalamu wa maabara kw4nye eneo la mpaka wa Namanga amesema shughuli za upimaji kwenye mpaka mara nyingi huenda polepole, na changamoto ni idadi kubwa ya watu wanaofika mpakani.

Keya ameeleza kwamba zoezi la kuchukua sampuli na upimaji wa sampuli zilizochukuliwa linaweza kuchukua muda wa siku mbili, pamoja na siku nyignine tatu wanazohitaji madereva wa malori kukamilisha masuala ya forodha na uhamiaji kwa jumla ni kama wiki nzima,  na hali hiyo ndio chanzo cha kuongeza uwezekano wa watu kuambukizana.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ilisema mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei kwamba inadhamiria kuwafuatilia madereva wa malori kupitia simu zao za rununu na kuwapa vyeti vya kuthibitisha kuwa wako salama kiafya. Lakini hatua hiyo haiwezi kutekelezwa hadi pale kila nchi itapoweka ofisi ya kuratibu na pia  nchi zote husika zitakapopata vifaa maalum vinavyohitajika, na kutokana na sababu hizo bado tarehe rasmi ya kuanza kwa zoezi hilo haijatangazwa. 

Hata hivyo kwa mujibu wa mtandao wa madereva kilio cha madereva wa malori katika eneo la Afrika Mashariki bado kipo palepale kwamba wengi wao wamekuwa wanatendewa vibaya wakati. Mtandao huo wa madereva umesema ni muhimu watu kutambua kwamba hata madereva wa malori ni binadamu kwa wengine na wana hofu ya kuambukizwa virusi vya corona na watu wengine.

Chanzo:/AP