Umoja wa Mataifa wasema Afrika Magharibi kukabiliwa na njaa
28 Mei 2020Katika nyakati za kawaida kabla ya janga la virusi vya Corona, Boureima Diawara anayefanya biashara ya kuuza maembe anasema, alikuwa akichukua siku tatu kusafirisha bidhaa hizo kutoka kusini mwa nchi ya Mali hadi Dakar, mji mkuu wa Senegal, safari yenye umbali wa kilomita 1,200.
Lakini tangu kuwekwa kwa vizuizi vya kudhibiti virusi vya Corona katika nchi za Afrika Magharibi, Diawara anaeleza kuwa, sasa anachukua zaidi ya siku 6. Isitoshe, baada ya kuchelewesha katika mipaka pamoja na zuio la kutembea usiku nchini Senegal, wafanyakazi wake wanalazimika kutupa magunia ya maembe yaliooza majalalani.
Vizuizi viliowekwa na serikali za Afrika Magharibi kupambana na COVID-19 vimeyumbisha biashara ya bidhaa zinazoharibika kwa haraka pamoja na biashara ya mifugo.
Umoja wa mataifa umeonya kuwa kukwamisha kwa biashara kunaongeza wasiwasi wa kutokea kwa uhaba wa chakula katika eneo la Afrika Magharibi. Shirika hilo la kimataifa linasema janga la COVID-19 huenda likasababisha kuongezeka mara mbili kwa idadi ya wakaazi wa Afrika Magharibi wenye ukosefu wa chakula kufikia watu milioni 43 katika kipindi cha miezi sita zijazo.
Kwa mujibu wa data za Kamati ya Kudumu ya Kudhibiti ueneaji wa jangwa katika eneo la Sahel, wafanyabiashara wa bidhaa zinazoharibika kwa haraka wamepata khasara ya asilimia 10.
Kadhalika data hizo zimeonyesha kuwa wale wanaojishughulisha na biashara ya mifugo wamekabiliwa na asilimia 30 ya khasara katika biashara yao.
Shughuli zakwamishwa
Wakati huo huo, utafiti wa wafanyabiashara wa mifugo, Afrika Magharibi umebaini kuwa kwa sasa asilimia 42 ya shuguhuli za kiuchumi kwa wafugaji zimesitishwa.
Mnamo Machi, Mauritania ilifunga mpaka wake na Senegal ambayo ndio soko kuu la mifugo yake. Hata kama mizigo na bidhaa mbalimbali inaruhusiwa kupita. Lakini kwa upande wa wafugaji, wizara ya kilimo ya Mauritania inasema inashikilia msimamo wake wa kutowaruhusu wafugaji ha mifugo yao hadi nchini Senegal
Nako nchini Benin, wafanyabiashara walikuwa tayari wanakabiliwa na changamoto hata kabla ya vizuizi vya kudhibiti Corona kuwekwa.
Hii ni kufuatia Nigeria kufunga mpaka wake na nchi hiyo mnamo Agosti mwaka uliopita kutokana na kile serikali ya rais Muhammadu Buhari ilisema ni kukabilana na magendo katika mpaka huo.
Hatahivyo, katika wiki za hivi karibuni, baadhi ya serikali zimeanza kulegeza vizuizi kama mojawapo ya hatua kuzuia kuporomoka kwa uchumi ikiwemo kufungua masoko na kupunguza muda wa marufuku ya kutembea.
Mkrugenzi mkuu wa kilimo, fedha na maendeleo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB, Atsuko Toda amezisifu serikali hizo kwa kupunguza vizuwizi vya usafirishaji wa chakula kutoka mataifa yao hadi ya Kigeni. Mtaalmu huyo ameeleza kuwa hatua hiyo ni ishara ambayo itaweza kuzuia kupanda kwa bei ya chakula na hivyobasi kuziuia janga lingine la uhaba wa chakula kama ambavyo ilitokea mnamo mwaka 2007-2008.
Katika eneo la Afrika Magharibi, biashara ya chakula, kwa kiasi kikubwa huendeshwa na wafanyabiashara wenye biashara ndogo ndogo ambao huuza bidhaa ikiwemo kuku, vitungu, ndizi nakadhalika. Wafanyabiashara hao hutumia usafiri wa umma kusafirisha mifugo kutoka nchi moja hadi nyingine.
Chanzo: Reuters