Corona: Uganda yaanza zoezi la utoaji chanjo
10 Machi 2021Hata hivyo baadhi ya wananchi wana mashaka kwamba hatua hii itawafanya watu kulegeza hatua za tahadhari. Hii ni kwa sababu hawajahamasishwa ipasavyo kwamba lazima waendelee kufanya hivyo kwa kuvaa barakoa na kujitakasa.
Wafanyakazi wa afya wapatao laki moja na nusu hii ndio wameanza kupata chanjo hiyo kote nchini ili baadaye wahusike katika kutoa chanjo hiyo kwa askari wa vyombo vya usalama, walimu na watu ambao wamelezewa kuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa kama vile wazee.
Waziri wa afya Jane Ruth Aceng pamoja na katibu wa kudumu katika wizara hiyo wamekuwa miongoni mwa wale waliopata chanjo hiyo katika hospitali kuu ya Mulago ambako zoezi hilo limezinduliwa rasmi.
Dianah Atwine ambaye ni katibu wa kudumu amesema hivi wakati akidungwa chanjo hiyo: "maumivu ya kudungwa yanastahimilika, hayana shida kwani siku zote tumekuwa tukidungwa sindano kwa hiyo si jambo la kuhofia."
Uganda imepokea shehena ya dozi 864,000 ya Astra Zeneca
Uganda ilipokea shehena ya dozi 864,000 aina ya Astra Zeneca kutoka kwa jumuiya ya wafadhili wiki iliyopita na siku mbili zilizopita ikapokea msaada wa dozi laki moja kutoka kwa serikali ya India. Hii ina maana kuwa angalau watu laki nne na nusu watabahatika kupokea chanjo hiyo.
Hii imeleta mashaka kwa idadi kubwa ya watu kwamba huenda umma utaanza kupuuza kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 wakisahau kuwa wanatakiwa kuendelea kuvaa barakoa, kudumisha umbali baina yao na na pia kujitasa au kunawa mikono kila mara.
Dorcas Onyango ni mwanahabari amesema: "Baada ya kupata chanjo hiyo ambayo ni kidogo ikilinganishwa na idadi ya watu, watu wtadhani tumepata dawa yenyewe, watapuuza kanuni hiyo inamaanisha natakiwa nibaki nikijilinda huku tukiendelea kuhamashishwa kutii kanuni."
Lakini waziri wa afya Jane Ruth Aceng ametahadharisha dhidi ya watu kupuuza kanuni ambazo wamezingatia kwa muda mrefu. Amewahimiza wananchi kuendelea kujilinda licha ya kuwa angalau kuna matumaini kwamba chanjo hii itapunguza kasi ya maambukizi.
"Uganda inaweza kupata wimbi jingine la mripuko kwa hiyo lazima sotetujichunge kwani hii imeshuhudiwa hata katika mataifa ambako utoaji chanjo unaendelea."
Naye mtaalamu wa masuala ya miripuko na chanjo Daktari Monica Musenero amewakumbusha watakaopata chanjo kwamba awali wataweza kuathirka kwa namna moj au nyingine kwa kuhisi, maumivu homa na joto la juu lakini watulize hali hiyo kwa kumeza dawa za kawaida.
"Pengine jioni hiyo utahisi homa kidogo. Hiyo ni ishara kwamba mwili wako umepokea chanjo hiyo hayo ni madhara ambayo yanaonyesha kwamba chanjo inafanya kazi mwilini."
Haijulikani kama baada ya Uganda kuanza kutoa chanjo kwa raia wake, itaruhusu ubalozi wa Marekani kuafanya hivyo kwa wafanyakazi wake ambao ni raia wa Uganda. Hapo awali, serikali ya Uganda ilikuwa imeukataza ubalozi huo kufanya hivyo.