Copa America-Brazil yailaza Chile 3:0
2 Julai 2007Copa America:baada ya kuzabwa mabao 2:0 na Mexico,Brazil ilijipatia jana ushindi wake wa kwanza katika kinyan’ganiyro cha kombe hilo ilipoitimua Chile kwa mabao 3:0.Mabao yote 3 yalitiwa na chipukizi wao anaeichezea Real Madrid Robinho.Mexico lakini haikuregeza kamba kwani nayo imekata tiketi yake ya robo-finali ilipoishinda Ecuador 2:1.Sasa Mexico wanaongoza kundi B kwa pointi 6 wakifuatwa na Brazil.
Uruguay na wenyeji Venezuela nao walinyakua ushindi wao wa kwanza katika Copa America hapo jumamosi ingawa mechi zote mbili ziligubikwa na ngware na maamuzi ya kutatanisha ya rifu.Uruguay iliichapa Bolivia bao 1:0 wakati wenyeji Venezuela walikumta Peru 2:0.
Ikijiandaa kwa msimu mpya ,mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani-Bayern Munich walifunga safari mwishoni mwa wiki hadi Hong Kong,China kuizaba Sao Paulo ya Brazil mabao 2:1.Ilikua sao Paulo lakini iliotangulia kutia bao .Mshambulizi mpya wa B.Munich Miroslav Klose alietia mabao mengi kabisa katika kombe lililopita la dunia akasawazisha kabla hamit Altitop,aliejiunga na Mumnich kutoka Schalke kuipatia Munich bao la ushindi.
Saudi Arabia ikijiandaa kwa Kombe la Asia linaloanza wiki ijayo Julai 7,imenyakua ubingwa wa mashindano yalioandaliwa Singapore licha ya kulazwa na Oman kwa mikwaju ya penalty baada ya kutoka sulhuhu bao 1:1.
Saudi ilibuka juu ya timu nyengine 4 baada ya kwanza kuwalaza wenyeji Singapore 2-1 na baadae kutoka suluhu na Oman.Wasaudi wako kundi moja na Bahrein,Korea ya kusini na wenyeji Indonesia.watafungua dimba na wenyeji wengine Korea ya kusini hapo julai 11.Oman itakutana na Australia,Iraq na Thailand.