COP25: Wito watolewa kuhusu mabadiliko ya tabianchi Madrid.
7 Desemba 2019''Wakati wa kuchukuwa hatua'' ndio kauli mbiu ya kongamano hilo la Umoja wa Mataifa la COP25 na matakwa yaliotolewa na baadhi ya waandamanaji elfu 500 walipoandamana katika barabara katika eneo la Kati mwa Madrid. Wanaharakati wa mazingira waliokuwa wakipiga na kucheza muziki walifanya familia zilizokuwa na watoto kujiunga nao huku watu wa matabaka mbali mbali wakikusanyika kuandamana katika mazingira yalioonekana kama tamasha.
Lakini ujumbe ulikuwa wazi kabisa:'' Hatua za hali ya hewa sasa'', ilisoma bango moja. '' Dunia moja ni sawa na fursa moja'', ikasoma bango jingine.
Kulingana na Danny, msichana wa umri wa miaka 15 aliyesafiri kutoka Colombia na wazazi wake, ameliambia shirika la habari la DW kwamba serikali zinapuuza masuala ya hali ya hewa na kwamba zinazingatia tu maslahi yao ya kibinafsi na sio maslahi ya vizazi vijavyo. Matamshi yake yaliunga mkono yale ya mwanaharakati wa mazingira kutoka Sweden Greta Thunberg. ''Watu wanataka kila kitu kiendelee kama sasa, na wanaogopa mabadiliko na mabadiliko ndio kile sisi vijana tunaleta,'' ameendelea kusema . ''Ndio maana wanataka kutunyamazisha, na huo ni ushahidi kwamba tuna ushawishi, kwamba sauti zetu zinasikika , kwamba wanajaribu sana kutunyamazisha.''
Maandamano ya siku ya Ijumaa yalifanyika maili chache kutoka eneo ambapo waakilishi kutoka kote duniani wanakutana katikamkutano wa zaidi ya wiki mbili katika kongamano la Umoja wa Mataifa la COP25 kuzungumzia hatua za kupunguza utoaji wa gesi chafu kama sehemu ya makubaliano ya Paris. Chini ya makubaliano hayo yaliothibitishwa na takriban mataifa 200, mataifa yalijiwekea malengo yao wenyewe ya kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa lengo la kupunguza ongezeko la joto duniani kufikia chini ya nyuzi 2 ikilinganishwa na viwango vya kabla ya viwanda kufikia mwisho wa karne hii.
Katika miaka hiyo minne tangu kufanyika kwa makubaliano hayo mwaka 2015, majadiliano yamekuwa yakiendelea kuhusiana na kile kinachoitwa, '' Kitabu cha muongozo'' - seti ya kanuni ambazo zitaongoza utekelezaji wa makubaliano ya Paris yanayotarajiwa kutekelezwa mwaka ujao.
Lakini malumbano miongoni mwa mataifa kuhusu jinsi ya kufuatilia utoaji wa gesi ya kaboni na masoko yake yametatiza hatua hiyo.Ufadhili wa kuyasaidia mataifa yanayoendelea kuzingatia mabadiliko ya tabianchi na kulipia uharibifu ambao umepatikana pia ni suala muhimu katika majadiliano hayo. Wakati huo huo, wataalamu wamesema kuwa malengo yakitaifa ya kupunguza utoaji wa gesi chafu hayana mkazo sana kuambatana na makubaliano ya Paris na huenda yakashuhudia kuongezeka kwa viwango vya joto kwa takriban nyuzi 3.