Congo yasajili kisa kipya cha Ebola
8 Februari 2021Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, limesema wafanyakazi wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamegundua kisa kipya cha virusi vya Ebola, ikiwa ni takribani miezi sita baada ya mlipuko huo kutangazwa kuwa umemalizika.
Kisa hicho kimegunduliwa baada ya mwanamke mmoja aliyekuwa mke wa mtu aliyenusurika na ugonjwa wa Ebola, kutafuta matibabu katika kituo cha afya mjini Butembo, jimboni Kivu ya Kaskazini, mashariki mwa Kongo ambako mripuko huo ulianzia. Mwanamke huyo alifariki baadae na majibu kuonyesha kuwa aliugua ugonjwa wa Ebola. Wafanyakazi wa afya wanaendelea kuwafuatilia zaidi ya watu 70 ambao wanaweza kuwa wamewasiliana na mwanamke huyo.
''Ndugu zangu wa Butembo wabaki watulivu''
Waziri wa Afya wa Kongo, Eteni Longondo amesema tayari wafanyakazi wa afya wamepelekwa kwenye eneo hilo ili kukadiria mahitaji na juhudi za kupambana na kuzuka upya kwa kirusi cha Ebola. Hata hivyo, serikali haikuelezea ikiwa ni janga jipya la ugonjwa wa Ebola au hapana.
''Nataka kuwambia ndugu zangu wa Butembo kwamba wabaki watulivu kwa sababu tulichukuwa hatua muafaka ili kukabiliana na ugonjwa huo. Timu ya wahudumu wa afya tayari imewasili huko na timu nyingine kutoka Kinshasa inatarajiwa pia kuwasili mwanzoni mwa wiki.'',alisema Longondo.
Congo tayari yakabiliwa na majanga 11 ya Ebola
Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO limesema kwamba wafanyakazi wake wamekuwa wakiyasafisha maeneo yote yaliYotembelewa na mwanamama huyo aliyefariki kutokana na Ebola. WHO imesema sio jambo la kushangaza kuona visa vya hapa na pale vinajitokeza baada ya janga kubwa lililodumu kwa miaka miwili.
Kisa hicho kimezuka baada ya serikali kutangaza kumalizika miezi mitatu iliyopita kwa ugonjwa wa Ebola kwenye jimbo lingine la Equateur, magharibi mwa nchi. Jimboni Equateur ugonjwa huo ulisababisha vifo vya watu 55 miongoni mwa 130 walioripotiwa kuambukizwa.
Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Kongo ulidumu kwa karibu miaka miwili na kuwaua jumla ya watu 2,299 na wengine 1,162 walipona. Ili kupambana na janga hilo serikali ya Kongo na Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO vilitoa chanjo kwa zaidi ya watu laki tatu na ishini elfu.
Chanjo hizo zilitengenezwa na makampuni ya Merck na Jonhson& Jonhson. Chanjo hiyo ilitumiwa pia jimboni Equateur. Tangu kuripotiwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976, ugonjwa wa Ebola, umezuka mara 11 nchini Kongo.