1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton afanya mazungumzo na Rais Sirleaf wa Liberia

Kabogo Grace Patricia13 Agosti 2009

Clinton ameahidi kumuunga mkono rais huyo pekee mwanamke barani Afrika.

https://p.dw.com/p/J97t
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton.Picha: AP

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton amewasili nchini Liberia, ikiwa ni kituo chake cha sita katika ziara yake ya siku 11 kwenye mataifa 7 ya Afrika. Jioni hii, Bibi Clinton anakutana na Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, rais pekee mwanamke barani Afrika aliyechaguliwa kidemokrasia, ambapo ameahidi kumuunga mkono.

Bibi Clinton ambaye atakutana pia na maafisa wa ngazi za juu wa Liberia na wabunge wa nchi hiyo, aliwasili kwenye uwanja wa ndege wa Monrovia huku kukiwa na mvua, lakini umati mkubwa wa watu ulijipanga kando kando mwa barabara kumpokea afisa huyo wa juu wa Marekani. Watoto wa shule walikuwa wameshika mabango yenye ujumbe unaosema ''karibu Clinton'', huku wanawake wakiwa wamebeba mabongo yenye ujumbe usemao ''Hillary Clinton--Wanawake wa Liberia tunakusalimu''

Bibi Clinton aliyewasili nchini Liberia akitokea Nigeria, alielekea kwenye mkutano baina yake na Rais Sirleaf, mwenye umri wa miaka 70, aliyechaguliwa mwaka 2005.

Nchi ya Liberia iliyoanzishwa na watumwa wa Marekani walioachiwa huru katika karne ya 19, ni nchi muhimu kwa Marekani kutokana na uchimbaji wa mafuta. Nchi hiyo ya Afrika Magharibi inapigania kujijenga upya baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1989 hadi 2003, vilivyosababisha vifo vya watu 300,000. Kwa sababu ya historia yake tangu Liberia ilipopata uhuru wake mwaka 1847, nchi hiyo imekuwa na uhusiano muhimu na Marekani.

Waziri huyo wa Nchi za Nje wa Marekani amewasili Liberia akitokea Nigeria ambako alitoa wito kwa serikali ya nchi hiyo kuwa na utawala bora, kumaliza tatizo la rushwa na kuwepo mshikamano zaidi baina ya Waislamu na Wakristo. Pia alielezea umuhimu wa utawala bora katika suala zima la uwekezaji.

Rais Sirleaf amekuwa akiungwa sana mkono na nchi za Magharibi, hasa Marekani, ambapo anaendeleza jitihada za kuijenga upya nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Johnnie Carson, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje kwa masuala ya Afrika, amesema Bibi Clinton anataka kuonyesha uungaji mkono kwa Rais Sirleaf.

Lakini mapema mwaka huu, Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Liberia, ilipendekeza rais huyo wa Liberia azuiwe kushiriki katika shughuli za kisiasa kwa miaka 30 kwa tuhuma za kuhusika katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kati ya mwaka 1989 na 2003. Rais Sirleaf alikiri kukutana kwa mara kadhaa na Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor na kusaidia kuchangisha fedha kwa ajili yake, lakini amekanusha kuwahi kuwa mjumbe wa chama cha Taylor cha National Patriotic Front for Liberia.

Bibi Clinton anatarajiwa kuhitimisha ziara yake hiyo mataifa saba barani Afrika kwa kuzuru Cape Verde, kabla ya kurejea Washington hapo kesho Ijumaa. Ziara yake hiyo ilizihusisha pia nchi za Kenya, Afrika Kusini, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman