080910 USA Koranverbrennung
8 Septemba 2010Mchungaji mmoja katika jimbo la Florida , kutokana na chuki dhidi ya Uislamu ,anataka siku ya Septemba 11 kukichoma moto kitabu kitakatifu cha Waislamu cha korani. Kitabu cha Korani ni kitabu kitakatifu kabisa kwa Waislamu ambapo hukiheshimu sana hata wanapokishika. Kukidharau kitabu hicho ni hatua mbaya kabisa na siku za nyumba hali kama hiyo imesababisha kutokea ghasia.
Septemba 11 jioni saa moja hadi saa tatu usiku , ni siku ya kukichoma kitabu cha Koran , maandishi hayo yapo katika gari iliyoegeshwa kando ya kanisa la mchungaji Terry Jones katika eneo la Gainesville mjini Florida.
Tunataka kuwakumbuka wale waliouwawa kinyama katika siku ya Septemba 11. Na kwa kweli tunataka kutoa ujumbe wa wazi kwa Waislamu wenye imani kali, kwamba hatuna haja na sharia, hatutaki maridhiano na vitisho vyao, woga wao na imani yao kali.
Anasema hayo mchungaji Terry Jones, ambaye anaongoza waumini 50, wa kundi la kanisa lijulikanalo kama "njiwa anayewafikia watu wote duniani" The Dove World Outreach, katika eneo la Gainesville , Florida, katika kuichoma Koran kama sehemu ya upinzani wao dhidi ya Uislamu wa imani kali. Kundi hilo ni moja kati ya makanisa madogo madogo yasiyo na idadi nchini Marekani , ambayo yamejitenga kutoka katika makanisa ya kiprotestanti. Jones pamoja na wafuasi wake wanasema kuwa wanatambua kile kitakachotokea kutokana na hatua waliyoipanga. Mchungaji huyo anasema kuwa tukio hilo litafanyika hata baada ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton kushutumu vikali mipango hiyo kuwa ni ya kuchukiza na dharau.
Nimefarijika kutokana na shutuma kali zilizotolewa dhidi ya kitendo hicho cha dharau na kinachochukiza cha kuchoma kitabu cha Koran, kutoka kwa viongozi wa Marekani wa imani zote, kutoka kwa Wakristo, Wayahudi , pamoja na viongozi wa serikali wasio upande wowote, pamoja na wale wenye ushawishi.
Clinton ni afisa wa ngazi ya juu kabisa wa serikali ya Marekani kuzungumzia dhidi ya kuchomwa kwa kitabu kitakatifu cha Koran. Ikulu ya Marekani ya White House imeongeza sauti yake katika tahadhari kuwa hatua hiyo inaweza kuzusha hasira katika ulimwengu wa Waislamu duniani na kuhatarisha maisha ya wanajeshi wa Marekani.
Hatua hii inayaweka majeshi ya Marekani katika hatari. Na ni dhahiri kuwa hatua yoyote kama hiyo inayoyaweka majeshi yetu katika hatari, inaiweka serikali yetu katika wasi wasi, amesema msemaji wa ikulu ya Marekani Robert Gibbs jana Jumanne.
Alikuwa akisisitiza maneno ya kamanda mkuu wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan , jenerali David Petraeus, ambaye alionya kuwa kukichoma kitabu cha Koran kutatoa nafasi kwa propaganda ya wapiganaji.
Licha ya kuwa idara ya zima moto imekataa kutoa kibali wiki chache zilizopita kwa ombi la mchungaji Jones, polisi hawawezi kuingilia kati hadi pale kitendo chenyewe kitakapofanyika cha kuchona nakala 200 za kitabu cha Koran.
Mwandishi : Albrecht Ziegler / ZR/ Sekione Kitojo/ AFPE
Mhariri : Mwadzaya,thelma