Uchumi wa kanda ya Ulaya utakuwa bora zaidi mwaka huu
19 Januari 2023Lagarde ameyasema haya huko Davos Uswisi kunakoendelea kongamano la uchumi duniani wakati ambapo kuna matumaini ya nchi kukwepa mdororo wa uchumi. Mkuu huyo amesema kwa sasa gumzo Ulaya si kudorora kwa uchumi tena, bali "kunywea kidogo" huku mataifa yenye uchumi mkubwa kama Ujerumani yakikwepa kabisa kunywea huko kwa uchumi wao.
"Kivyovyote vile, haijalishi unavyoutazama, mfumko wa bei uko juu sana na nia yetu katika Benki Kuu ya Ulaya ni kuurudisha hadi asilimia mbili kwa wakati mzuri na kuchukua hatua zote tunazostahili kuchukua ili kutimiza hilo," alisema Lagarde.
Benki Kuu ya Ulaya yatarajia ukuaji wa uchumi katika kanda ya Ulaya kwa asilimia 0.5.
Kulingana na makadirio yake, Benki Kuu ya Ulaya inatarajia kuwepo na ukuaji wa uchumi katika kanda ya Ulaya kwa asilimia 0.5. Matumaini hayo ingawa yenye tahadhari yameanza wakati ambapo bei za juu za nishati zilizopanda mwaka jana kutokana na vita nchini Ukraine, zikiwa zimeanza kushuka.