China yatangaza ushuru wa dola bilioni 50 dhidi ya Marekani
16 Juni 2018Orodha hiyo ya China iliyotangazwa siku ya Jumamosi (16 Juni) inajumuisha asililimia 25 ya ushuru wa forodha kwa aina 659 ya bidhaa zikiwemo za kilimo, magari na majini, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya fedha ya China ambayo, hata hivyo, haikufafanuwa zaidi kuhusu bidhaa zenyewe hasa.
Ushuru kwa bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 34 utaanza kutekelezwa tarehe 6 Julai, siku ambayo ndiyo Marekani iliyotangaza kuanza kutolesha ushuru bidhaa kutoka China. Ushuru wa dola 16 zilizosalia utatozwa siku zijazo.
Wizara hiyo ya fedha ya China imekosoa vikali hatua za Marekani kuweka ushuru mpya ikisema zinavunja kanuni za Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) na kwamba hatua zake za kulipiza kisasi ni kwa ajili ya "kulinda haki na maslahi halali kwa mujibu wa misingi ya sheria za kimataifa."
"China haitaki kupigana kwenye vita vya kibiashara, lakini kwa kukabiliwa huku na ukosefu wa kuona mbali wa Marekani, China inalazimika kulipiza vikali," ilisema taarifa ya wizara ya biashara.
Wizara hiyo pia iliongeza kuwa inavunja makubaliano ya kupunguza ziada kwenye biashara ya mabilioni ya dola na Marekani kwa kununuwa zaidi bidhaa za kilimo, gesi asilia na bidhaa nyengine.
Hatua za Marekani
Nyingi ya bidhaa hizi ni chakula na za mashambani, na hatua hii itawaumiza sana waungaji mkono wa Trump wanaoishi maeneo ya vijijini. China inaonekana kuchaguwa kuachana na bidhaa ambazo zinaweza kubadilishwa kirahisi na zile ambazo zinaingia kutoka Brazil na Australia.
Kuna uwezekano pia wa kuwekwa ushuru mpya kwa bidhaa nyengine zipatazo 114, vikiwemo vifaa vya matibabu na bidhaa za nishati, kwa mujibu wa wizara ya fedha ya China, ingawa iliongeza kuwa orodha kamili ingelitangazwa siku zijazo.
Uamuzi huu wa China unafuatia ule wa Marekani wa siku ya Ijumaa (Juni 15), ambapo utawala wa Trump ulitangaza ongezeko la ushuru wa dola bilioni 34 kwa bidhaa kutoka China na mipango ya kutangaza nyengine bilioni 16 kwa bidhaa nyenginezo hapo baadaye.
Trump anaishinikiza China kupunguza uzalishaji wa ziada kwenye biashara na marekani na kuachana na mipango yake ya kuwafadhili washindani wa kibiashara duniani katika sekta za teknolojia yakiwemo magari ya umeme, nishati jadidifu, uvumbuzi wa kibaiolojia na kompyuta.
Marekani, Ulaya, Japan na washirika wengine wa kibiashara wanalalamikia mbinu za China zikiwemo zile za wizi wa teknolojia ya kigeni na utoaji ruzuku na ulinzi dhidi ya ushindani kwa viwanda vyake. Washirika hao wanadai kuwa hatua hizo za China zinavunja ahadi yake ya soko huria chini ya WTO.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP
Mhariri: Bruce Amani