1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yamuwekea vikwazo Pelosi

5 Agosti 2022

China imetangaza kumuwekea vikwazo spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi kufuatia ziara yake ya Taiwan mwanzoni mwa wiki.

https://p.dw.com/p/4FAWA
Nancy Pelosi hält Pressekonferenz in Tokio
Picha: Issei Kato/REUTERS

 China imetangaza kumuwekea vikwazo spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi kufuatia ziara yake ya Taiwan mapema wiki hii. Haya yanafanyika wakati ambapo Taiwan imeishutumu China kwa kukizingira kisiwa hicho na kufanya luteka za kijeshi zilizolaaniwa na Marekani na nchi za Magharibi.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya China iliyotolewa Ijumaa imesema kwamba Pelosi alipuuzilia mbali wito wa China wa kumtaka asikizuru kisiwa hicho ambacho China inasema kiko chini ya himaya yake na inapinga ushirikiano wake na nchi za kigeni.

Ni kutokana na hatua hiyo ndiyo China sasa imemuwekea vikwazo hivyo ambavyo haikuviweka wazi. Pelosi ndiye aliyekuwa afisa wa ngazi ya juu wa Marekani kukizuru kisiwa hicho katika kipindi cha miaka 25.

Ziara ya Pelosi yatumiwa kama kisingizio cha kuivamia Taiwan

Haya yanafanyika wakati ambapo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema Ijumaa kuwa luteka za kijeshi za China kwa Taiwan yakiwemo makombora yaliyorushwa katika eneo la kipekee la kiuchumi la Japan, yanaashiria upanuzi wa mvutano huo na ameitaka China kupunguza luteka hizo.

Kambodscha | ASEAN Gipfeltreffen: Antony Blinken und Sergei Lawrow
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani akiwa katika mkutano wa ASEANPicha: Andrew Harnik/AP/picture alliance

"Jeshi la ukombozi sasa limetangaza maeneo saba yenye vikwazo karibu na Taiwan na limesema litaongeza luteka za kijeshi hadi Jumatatu. Uchokozi huu ni kuzidi kuupanua mvutano," alisema Blinken.

Blinken amesema China inatumia ziara ya Pelosi kama kisingizio cha kuzidisha luteka zake za kijeshi ndani na katika kisiwa cha Taiwan. Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani amewaambia waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano wa Mataifa ya Kusini Mshariki mwa Asia ASEAN huko Cambodia kuwa, ziara ya Pelosi ilikuwa yenye amani na haikuwakilisha mabadiliko yoyote ya sera ya Marekani kwa Taiwan.

Ndege za kivita na meli za China zavuka "mstari wa median"

Nalo gazeti la washington Post limeripoti Ijumaa kwamba Ikulu ya White House ilimuita balozi wa China Qin Gang jana, ili kulaani vitendo vya China kwa Taiwan na kumsisitizia kwamba Marekani haitaki mgogoro katika eneo hilo.

China | PLA Kampfjet über Pingtan
Ndege ya kivita ya China ikiruka juu ya kisiwa cha Pingtan kuelekea TaiwanPicha: ALY SONG/REUTERS

China imesema kwamba luteka zake zitaendelea hadi Jumapili mchana nayo Taiwan imeripoti kuwa meli na ndege za kivita za China zimevuka "mstari wa median" ambao ni mpaka usio rasmi ila uliokuwa unaheshimika sana wakati mmoja, unaoitenganisha China na Taiwan.

China imekuwa ikifanya uvamizi wa mara kwa mara tangu mwaka 2020 ilipotangaza kwamba mpaka huo usio rasmi hautumiki tena. Waandishi wa shirika la habari la Ufaransa AFP katika kisiwa cha China cha Pingtan wamesema wameona ndege ya kivita ya China ikiruka juu ya kisiwa hicho jambo lililowafanya watalii kupiga picha.

Chanzo:AFP/AP