1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yafanya luteka mpya za kijeshi Taiwan

8 Agosti 2022

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema Taiwan ni sehemu ya nchi hiyo na kwamba China inafanya luteka za kawaida za kijeshi katika eneo lake la baharí kwa uwazi na kutumia taaluma.

https://p.dw.com/p/4FFnW
Taiwan China Konflikt Manöver
Picha: Hector Retamal/AFP

Akizungumza Jumatatu na waandishi habari, msemaji wa wizara hiyo, Wang Wenbin amesema kuwa idara zinazohusika pia zimetoa matangazo kwa wakati na hiyo ni kwa mujibu wa sheria za ndani na za kimataifa.

Matamshi hayo ameyatoa baada ya kuulizwa na waandishi habari iwapo hatua ya China kuendelea na luteka ya kijeshi inaheshimu sheria za kimataifa au la, na ikiwa tahadhari mpya itatolewa kuhusu meli za raia na ndege za kijeshi.

China Jumatatu imeendeleza luteka mpya za kijeshi kuzunguka Taiwan, na kukaidi wito wa kusitisha mazoezi yake makubwa ya kijeshi kuwahi kushuhudiwa katika kisiwa hicho kinachojichukulia kuwa taifa huru, kutokana na ziara iliyofanywa na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi.

Taiwan in höchster Alarmbereitschaft: China führt Schießübungen durch
Hali bado ni tete Taiwan kutokana na mazoezi ya kijeshi ya ChinaPicha: Annabelle Chih/Getty Images

Wakati huo huo, Taiwan imesema itafanya luteka ya kijeshi baadae wiki hii kujilinda na uvamizi wa China. Taarifa iliyotolewa Jumatatu na maafisa wa Taiwan imeeleza kuwa kisiwa hicho kinachojitawala na cha kidemokrasia, kiko katika kitisho cha mara kwa mara cha kuvamiwa na China, ambacho inakichukulia kisiwa hicho kama himaya yake ambacho itakuja kukirejesha siku moja hata kwa njia za kijeshi ikibidi.

Luteka ya kijeshi ya Taiwan Jumanne na Alhamisi

Jeshi la Taiwan limesema kuwa viikosi vya kisiwa hicho vitafanya mazoezi hayo ya kijeshi katika eneo la Pingtung, siku za Jumanne na Alhamisi.

Kwa mujibu wa msemaji wa vikosi vya Taiwan, Lou Woei-jye, luteka hiyo itajumuisha kupelekwa mamia ya wanajeshi na takribani bunduki 40 aina ya Howitzer. Lou amesema mazoezi hayo tayari yalikuwa yamepangwa kufanyika na hayana lengo la kujibu luteka za kijeshi za China.

Taiwan Taipeh | Premierminister Su Tseng-Chang
Waziri Mkuu wa Taiwan, Su Tseng-changPicha: APTN/AP Photo/picture alliance

Waziri Mkuu wa Taiwan, Su Tseng-chang ameishutumu China kwa kufanya luteka za kijeshi kuvuruga amani katika ujia wa bahari ya Taiwan. ''Tunatoa wito kwa serikali ya China kuacha kutumia nguvu zake za kijeshi kuonyesha uwezo wake kila mahali na kuhatarisha amani katika ukanda huu,'' alifafanua Su siku ya Jumapili mbele ya waandishi habari.

China: Marekani inawajibika kufutwa mazungumzo ya kijeshi 

Huku hayo yakijiri, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China, Wu Qian amesema Jumatatu kuwa China imesema Marekani inapaswa kuwajibika kikamilifu kutokana na kufutwa kwa mazungumzo ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili.

Siku ya Ijumaa, wizara ya mambo ya nje ya China ilitangaza hatua nane za kuchukua kujibu ziara iliyofanywa na Pelosi mjini Taipei. Moja kati ya hatua hizo, ya kwanza ilikuwa kufutwa kwa mazungumzo ya kijeshi kati ya China na Marekani, ikijumuisha Mazungumzo ya Makamanda, Mazungumzo ya Uratibu wa Sera ya Ulinzi na Mazungumzo kuhusu makubaliano ya kijeshi katika eneo la bahari.

 

 

(AFP, Reuters)