China na Urusi zamkingia kifua Assad
20 Julai 2012Wakati katika mji mkuu Damascus machafuko yanazidi kuongezeka, Urusi na China Alhamis (19.07) zilitumia kura zao za veto dhidi ya azimio la umoja huo dhidi ya Syria. Hii ni mara ya tatu nchi hizo kutumia kura zao za veto. Azimio hilo lilikuwa na lengo la kuweka vikwazo dhidi ya utawala wa rais Bashar al-Assad.
Wakati rais wa baraza hilo Nestor Osorio kutoka Columbia alipowataka wanachama 15 wa baraza hilo kupiga kura kuhusu mswada wa azimio hilo, macho yote yaliwageukia wawakilishi wa Urusi na China. Na kama ilivyotarajiwa mikono yao ilikuwa tayari juu, ikiwa ni ishara ya upinzani wao.
China na Urusi zakinga kifua
Hii ni mara ya tatu, ambapo inazuwia hatua kali dhidi ya utawala wa Bashar al-Assad kwa kutumia kura zao za veto katika umoja wa mataifa. Balozi wa Uingereza katika umoja wa mataifa, Lyall Grant, amesema kuwa amesitushwa na uamuzi huo.
"Athari za matendo yao ni kuunga mkono utawala wa kikatili na wanaweka maslahi ya nchi zao mbele kuliko maisha ya mamilioni ya Wasyria."
Mwanadiplomasia huyo ambaye amekasirishwa na hatua hiyo amesema kuwa zaidi ya watu 14,000 wasio na hatia nchini Syria wameuwawa, tangu pale Urusi na China mwezi wa Oktoba mwaka jana zilipotumia kwa mara ya kwanza kura zao za veto kuukingia kifua utawala wa Assad. Mswada huo wa azimio ambao pia uliungwa mkono na Ujerumani, ambapo Pakistan na Afrika Kusini hazikupiga kura, ulipata kura 11 ambazo zingetosha kuupitisha kwa kura nyingi, ulikuwa unatishia kuuwekea vikwazo zaidi utawala wa Syria, iwapo utawala huo utaendelea kupinga mpango wa amani wa mjumbe wa kimataifa na wa jumuiya ya nchi za kiarabu kwa mzozo wa Syria, Kofi Annan.
Muda wa ujumbe kuongezwa
Pamoja na hayo kutokana na hali ya kuongezeka kwa ghasia nchini Syria, kundi la uangalizi la umoja wa mataifa linapaswa kuongezewa muda wa kukaa huko kwa siku 45. Azimio la aina hii ni kwa maslahi ya mataifa ya magharibi na kwamba ni kisingizio cha kutaka kuhalalisha mashambulio ya kijeshi, amesema balozi wa Urusi katika umoja wa mataifa, Vitaly Churkin.
"Vita vya mataifa mengine vinafanyika katika ardhi ya Syria, ambavyo havina uhusiano wowote na maslahi ya watu wa Syria."
Maelezo ya balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa, Susan Rice, yameonyesha kuwa upinzani huo ni kama wenda wazimu. Urusi imekuja na mswada wa azimio lake ambalo linataka kurefushwa kwa ujumbe wa umoja wa mataifa nchini Syria. Pakistan ikiungwa mkono na Urusi, inapendekeza kurefushwa kwa muda wa ujumbe huo wa umoja wa mataifa kwa siku 45. Uingereza inapendekeza kurefushwa huko kwa siku 30. Muda wa ujumbe huo umemalizika usiku wa manane leo Ijumaa. Kura inatarajiwa kupigwa leo.
Wakati huo huo, waasi nchini Syria wamedai kuwa wameviteka vivuko vya mpakani vya Syria kuingia Iraq na Uturuki. Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Iraq amesema wapiganaji wa jeshi la waasi la Syria huru wanadhibiti vivuko vyote katika mpaka wa nchi hizo mbili, na kuongeza kuwa Iraq imeufunga mpaka wake kufuatia ulipizaji kisasi wa waasi dhidi ya majeshi ya Syria.
Mwandishi : Schmidt, Thomas / ZR/ Sekione Kitojo
Mhariri: Josephat Charo