China na Urusi kuanza "enzi mpya" ya ushirikiano
17 Mei 2024Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenyeji wake wa China Xi Jinping wameahidi kuanza "zama mpya" ya ushirikiano katika kile kinachotafsiriwa kama kuungana pamoja dhidi ya mpinzani wao mkuu Marekani ambaye wanamuelezea kuwa mchochezi anayetaka kurejesha enzi za vita baridi na kusababisha machafuko kote duniani.
Rais Xi amempokea Putin kwa heshima zote za kiitifaki na kijeshi ikiwa ishara ya wazi ya kumuhakikishia kiongozi huyo wa Urusi kuhusu ushirikiano wao wa karibu, huku Xi akimueleza Putin kuwa uhusiano kati ya China na Urusi umepatikana kwa tabu na kwamba pande zote mbili zinapaswa kuutunza na kuuenzi.
Viongozi hao wawili wametia pia saini taarifa ya pamoja ambayo inadhihirisha wazi upinzani kwa Washington kuhusu mambo mbalimbali ya kiusalama na kimkakati, ikiwa ni pamoja na mvutano kati ya China na kisiwa cha Taiwan, vita vya Urusi nchini Ukraine, misimamo kuhusu Korea Kaskazini, mahusiano ya kibiashara na ushirikiano wa teknolojia mpya ya nyuklia.
Uhusiano usioyumba kati ya Beijing na Moscow
Itakumbukwa kuwa mnamo Februari mwaka 2022, China na Urusi zilitangaza azma yao ya kuwa na ushirikiano "usio na kikomo", wakati Putin alipotembelea Beijing siku chache kabla ya kuanza uvamizi wake nchini Ukraine ambao hadi sasa umesababisha vifo vingi zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Soma pia: Rais wa Urusi afanya ziara nchini China
Rais Putin amemshukuru mwenzake wa China Xi Jinping kwa juhudi za kutatua mzozo unaoendelea nchini Ukraine huku Xi akisema nchi yake inataraji bara la Ulaya litarejea hivi karibuni katika hali ya amani na utulivu na kuongeza kwamba China itatekeleza jukumu muhimu la kufanikisha hilo.
Xi amesema nchi yake iko tayari kushirikiana na Moscow ili kufikia maendeleo na ustawi wa pande zote na kwa pamoja wamejitolea kusimamia uadilifu na haki kote ulimwenguni. Rais huyo wa China amemueleza mwenzake wa Urusi kuwa mataifa hayo mawili yana nafasi ya kuleta mabadiliko ambayo katika karne nzima hayajawahi kushuhudiwa duniani. Wachambuzi wengi wameyatafsiri mabadiliko hayo kama jaribio la kupinga utaratibu wa sasa wa kimataifa unaoongozwa na Marekani.
Washington inaichukulia China kama mshindani wake mkubwa na Urusi kama tishio kuu kwa taifa hilo, huku ikiwachukulia Xi Jinping na Vladimir Putin kama viongozi wenye utawala wa kimabavu ambao wanakandamiza uhuru wa kujieleza na kudhibiti vikali vyombo vya habari na mihimili ya mahakama. Rais Joe Biden alithubutu hata kusema kuwa Xi ni "dikteta" na Putin ni "muuaji na mwendawazimu". Beijing na Moscow zililaani vikali kauli hizo.
(Vyanzo: RTRE, APE)