China na Marekani zatoa ahadi mpya za kukabili joto duniani.
24 Septemba 2021Viongozi wa nchi hizo mbili kubwa kiuchumi walitangaza hatua tofauti katika mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa ulioanza wiki iliyopita.
China, kwa upande wake, imeahidi kusimamisha ufadhili wa uchimbaji wa makaa ya mawe katika nchi za nje, huku Marekani ikitoa ahadi ya kufadhili maradufu hatua za kukabliana na janga la tabianchi katika nchi zinazoendelea.
Ahadi hizo zimesifiwa kama hatua muhimu kabla ya Kongamano la kujadili hali ya hewa la Umoja wa mataifa COP26, litakalofanyika mwezi Novemba mjini Glasgow.
Pamoja na hayo, vikundi vinavyoongoza kampeni za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi vimezidi kuzishinikiza Marekani na China, kwa hoja kuwa nchi hizo mbili kufanya mengi zaidi mnamo wiki zijazo.
Saleemul Huq, Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo nchini Bangladesh, alisema, ufadhili na hatua za kupunguza uzalishaji "vinahitaji kuongezwa pakubwa "kabla ya COP26.
Kuzitaka nchi kuimarisha hatua za kupunguza uzalishaji wa hewa chafu na kutoa fedha kusaidia mchakato mzima ni muhimu kabla ya kongamano hilo la COP26, linalotazamiwa kutoa nafasi ya mwisho ya kushawishi juhudi za pamoja za kupunguza joto duniani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha ahadi kutoka Marekani na China, lakini akazidi kusisitiza kwamba dunia nzima "inakazi kubwa ya kufanya ili kuyafikia malengo ya COP26".
Guterres amezihimiza nchi zote za Umoja wa Mataifa kuongeza juhudi zao na kuchukua mwelekeo mpya katika kongamano hilo muhimu luhusu utunzaji wa mazingira. Hii amesema Guterres, itakuwa muhimu katika jitihada za kutimiza lengo la kubakisha ongezeko la joto duniani chini ya nyuzi 1.5. Kiwango hiki kiliafikiwa mjini Paris mnamo 2015.
Kusitisha matumizi ya makaa ya mawe kunaonekana kufanikisha ahadi ya makubaliano ya Paris ya kukidhi ongezeko la joto duniani "chini" ya nyuzi 2 hadi 1.5C. Hii ikiwa muhimu katika kukabiliana na hathari za tabianchi kama vile dhoruba kali, mafuriko, moto wa mwituni na kufeli kwa mazao.
Wanaharakati walihimiza China kutoa ufafanuzi zaidi juu ya jinsi inavyopanga kumaliza ufadhili wa kuzalishi makaa ya mawe nje ya nchi, na kuweka ratiba wazi ya kumaliza matumizi ya nishati chafu nchini China kwenyewe.
"Hii ni muhimu kwani China, mfadhili mkubwa katika uzalishaji wa makaa ya mawe duniani, imeweka wazi kuwa uzalishaji haitakuwa mojawapo ya shughuli zake za usoni" alisema Joojin Kim, mkurugenzi mkuu wa shirika la Solutions for Our Climate, lenye makao yake Seoul.
Makaa ya mawe bado ni tegemeo la uzalishaji umeme huko Asia, ambayo inachangia asilimia 75 ya mahitaji ya makaa ya mawe ulimwenguni, kulingana na Shirika la Nishati la Kimataifa.
China peke yake ina idadi kubwa duniani ya kufanikisha uzalishaji wa umeme kupitia makaa ya mawe na hii ni kulingana na ripoti ya kikundi cha wataalamu cha E3G, iliyochapishwa mwezi Septemba.
Li Shuo, mshauri mwandamizi wa shirika la Greenpeace Asia Mashariki, alisema atakuwa akiangalia jinsi Beijing inavyotekeleza ahadi yake mpya, haswa jinsi itakavyotumika kwa benki za serikali na mashirika mengine.
"Kwa mwelekeo mpya uliowekwa kwa makaa ya mawe nje ya nchi, China inahitaji kufanya kazi kwa bidii sasa juu ya kutengemea makaa ya mawe," aliongeza. "Beijing inapaswa kupunguza kwa kiwango kikubwa makaa ya mawe katika mfumo wake wa nishati ili kuhakikisha kiwango chake cha uzalishaji kabla ya mwaka 2025."
Vikundi vya watetezi wa mazingira pia vilimsihi Rais wa Marekani Joe Biden ajitahidi zaidi baada ya kuiambia hadhara ya umoja wa mataifa kuwa atafanya kazi na Bunge kuongeza fedha za kusaidia miradi ya ulinzi wa mazingira kwa mataifa yanayoendelea hadi dola 11.4 bilioni kwa mwaka ifikapo 2024.
Vyanzo: rtre, afpe
Mwandishi: George Okach
Mhariri: Daniel Gakuba