1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Marekani zitashirikiana kupunguza gesi chafu

11 Novemba 2021

Mataifa mawili yanayoongoza kwa kuzalisha gesi chafu ulimwenguni, China na Marekani, yamekubaliana kuongeza ushirikiano na kuchukua hatua zaidi katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/42qVK
COP26 in Glasgow |  Xie Zhenhua
Picha: Alastair Grant/AP/picture alliance

Hatua hiyo inaashiria kuwa mataifa hayo mawili yako tayari kuweka tofauti zao kando, na kushirikiana kushughulikia tatizo la ongezeko la joto ulimwenguni.

Mjumbe wa China Xie Zhenhua na mwenziwe wa Marekani John Kerry wamesema mataifa hayo mawili yatashirikiana kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa viwango vilivyoridhiwa kwenye mkutano wa Paris wa mwaka 2015 wa mabadiliko ya tabinchi.

Soma zaidi: Makampuni sita ya magari kuahidi kuondoa magari yanayotumia mafuta 2040

Wajumbe hao walitangaza taarifa hiyo katika mikutano miwili tofauti na waandishi habari, iliyofanyika mjini Glasgow pembezoni mwa mkutano wa COP26.

Xie amesema kutolewa kwa tamko hilo la pamoja kunaonyesha kwamba ushirikiano ni njia pekee kwa China na Marekani kuonyesha uwajibikaji kwenye suala la uchafuzi wa tabala la hewa.

"Kwa kufanya kazi pamoja, Marekani na China zinaweza kufikia malengo mengi muhimu yenye manufaa si tu kwa nchi zetu mbili, bali kwa dunia nzima, kama mataifa mawili makubwa duniani, China na Marekani zina wajibu maalum wa kimataifa," amesema Xie Zhenhua.

COP26 in Glasgow | John Kerry
COP26 mjini Glasgow | John KerryPicha: Alastair Grant/AP/picture alliance

China na Marekani zitashirikiana licha ya tofauti zao

Naye John Kerry wa Marekani amesema makubaliano hayo ya ushirikiano yalianza kujadiliwa tangu mwanzoni mwa mwaka uliopita kati ya marais wa mataifa hayo mawili.

"Naamini licha tofauti zetu tulizonazo, ni muhimu sana kwetu kuzingatia machafuko ya kiulimwengu. Hili ni janga la uchafuzi wa hali ya hewa. Na ni mojawapo ya matatizo makubwa tunayokabiliana nayo duniani. Na nadhani ni jukumu letu kuchukua uamuzi huu," amesema John Kerry.

Serikali zilikubaliana mjini Paris kupunguza kwa uzalishaji wa gesi ya chafu ili kuhakikisha joto haliongezeki kwa zaidi ya nyuzi joto mbili ulimwenguni kote. Na kiwango kilicho bora ni kuhakikihsa joto halipandi kwa zaidi ya nyuzi joto 1.5.

Soma zaidi: Uchafuzi wa hewa kuongezeka tena mwaka huu

Lakini Xie amesema, pande zote mbili zinatambua kuwa kuna pengo kati ya juhudi zilizochukuliwa duniani kote kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa na malengo ya mkataba wa Paris. Hivyo ushirikiano wao utasaidia kuziba pengo hilo.

Tamko hilo la pamoja limetolewa siku chache baaada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuwalaumu marais wa China Xi Jinping n awa Urusi Vladimir Putin kwa kushindwa kuhudhuria mkutano huo wa COP26.

Aidha taarifa hiyo imesema kuwa Marekani na China zitaunda timu ambayo itakuwa ikikutana mara kwa mara kujadili hatua za kuchukua kupunguza uchafuzi wa hali ya hewa.

Vyanzo: (rtre, afp, ap)