China, EU zajenga matumaini ya kuikabili Marekani
10 Aprili 2019Matarajio ya mkutano wa kawaida wa kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang, yalitajwa yangekuwa finyu, huku ikiashiriwa kuwa pengine ungemalizika bila ya kupatikana maendeleo yoyote na hata taarifa ya pamoja ilitajwa na upande wa Umoja wa Ulaya kwamba pengine isingetolewa.
Lakini ujumbe wa China ulikwenda Brussels na ahadi mpya, ambazo ndizo zilizozinusuru pande hizo mbili na kuepusha balaa la kidiplomasia lililokuwa likihofiwa.
"Majadilianao yalikuwa magumu lakini mwishowe yameleta tija," alisema Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk, akiongeza kwamba "ushirikiano lazima uzingatie maslahi ya pande mbili".
Kwa kuzingatia hali ya kiuchumi namna ilivyo hivi sasa, Umoja wa Ulaya na China zingelifaidika zaidi na mfumo wa kibiashara unaofuata sheria.
Matamshi hayo yanagusia moja kwa moja vita vya kibiashara kati ya Marekani na China pamoja na vitisho kutoka Washington dhidi ya nchi za Umoja wa Ulaya.
Tangazo la ghafla la Rais Donald Trump wa Marekani kutaka kuzitoza ushuru wa dola bilioni 11 bidhaa zinazosafirishwa na nchi za Umoja wa Ulaya ili kufidia ruzuku zinazotolewa na serikali kwa kampuni ya kutengeneza ndege ya Airbus, nalo pia liligubika mazungumzo kati ya Li Keqiang na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.
China yaahidi kufungua milango kwa bidhaa za Ulaya
Pande hizo mbili zinakabiliwa na suala la maslahi ya kimkakati: nalo ni kama waendeleze aina fulani ya ushirikiano kutokana na shinikizo la Washington, au kila mmoja aendelee kupigania masilahi yake.
Kwa vyovyote vile Umoja wa Ulaya ndio mshirika mkubwa wa kibiashara wa China na kinyume chake China inakamata nafasi ya pili barani Ulaya.
Pande zote mbili zilikuwa na furaha ya kutangaza kwamba "maridhiano yamefikiwa".
Kwa mara ya kwanza, China ilikubali kushirikiana katika kulifanyia mageuzi Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO), kwa mujibu wa Tusk.
Naye Keqiang aliahidi pia kuwa kampuni za Ulaya zingetendewa sawa nchini China.
Lakini kwa umbali gani ahadi zilizotolewa kwa kampuni za Ulaya zingetekelezwa, hilo watu watabidi wasubiri ili waone.
China ilishawahi kutoa ahadi kama hizo, kwa mfano mwaka 2017 pale Rais Xi Jinping aliposema katika Kongamano la Kiuchumi Ulimwenguni mjini Davos nchini Uswisi kuwa China ingeliwacha wazi masoko yake.
Lakini paka leo hilo halijatekezwa!
Imetayarishwa na Barbara Wesel, DW