1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Homa ya manjano Congo Kinshasa

Admin.WagnerD17 Agosti 2016

Shirika la afya duniani WHO linatarajia kutoa chanjo ya ugonjwa wa homa ya manjano kwa wananchi wa Congo wapatao milion 8.5 katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa na wengine milion 3.4 waishio mipakani.

https://p.dw.com/p/1JjWn
Mwananchi wa Congo akipatiwa chanjo kwenye kampeni ya dharura dhidi ya homa ya manjano.Picha: Reuters/K. Katombe

Mlipuko wa ugonjwa huo umeua mamia ya watu katika ukanda wa Afrika ya kati licha ya kutarajiwa kuanza kwa kampeni kubwa ya kutoa chanjo. Awali ugonjwa huo uliripotiwa nchini Angola kabla ya kuenea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwezi June mwaka huu Congo ilitangaza mlipuko wa homa hiyo ambapo watu 360 wamefariki tangu mwezi Desemba mwaka jana ukiwa ni mlipuko mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo.

Pamoja ya kuripotiwa mpango wa kuanza kutoa chanjo kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa chanjo yenyewe na vifaa vingine kwa kuwa kiwango kikubwa kilitumika katika kukabiliana na milipuko ya ugonjwa huo ambayo imekuwa ikitokea mara kwa mara mwaka huu.

Utengenezaji wa chanjo za homa ya manjano huchukua mwaka mmoja na mpaka sasa kuna chanjo milioni saba tu zinazoweza kutolewa kwa hali ya dharura.

Heather Kirr Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Save the children nchini Congo amesema Kuna mahitaji ya dharura kwa sababu kuna watoto na familia nyingi ambazo zinahitaji kufikiwa licha ya kuwa kuna chanjo chache.

Impfung Afrika Gelbfieber
Msichana nchini Liberia akipata chanjoPicha: picture-alliance/dpa

Hatari ya kuenea mataifa mengine duniani

Homa ya manjano, ugonjwa ambao hauna tiba inayofahamika mpaka hivi karibuni unaweza kuenea katika maeneo mengine duniani. Kwa mujibu wa WHO kuna visa 2,269 na vifo 16 vimeripotiwa mwezi huu

Nae mkurugezi wa zamani wa kitengo cha dharura cha shirika la afya duniani WHO Dr. Bruce Ayward anasema majanga kama haya yanapotokea kusaidia Serikali na taasisi nyingine kujipima jinsi ambavyo zinaweza kukabiliana nayo

Nchini Angola kampeni ya kutoa chanjo kwa watu milion 3.4 inaanza wiki hii pamoja na kuwa WHO imesema ugonjwa huo huenda umedhibitiwa kwani hakuna ripoti za maambukizi mapya iliyotolewa nchini humo tangu mwezi juni.

Homa ya manjano, ni ugonjwa unaouwa ambao huenezwa na mbu, hasa wa aina ya Aedes.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/ Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel