Chanjo kwa ajili ya watoto Milioni 300
28 Januari 2015Waziri wa Ujerumani anaeshughulikia ushirikiano wa maendeleo Gerd Müller amesema hadi kufikia mwaka wa 2030, hakuna mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano atakeachiwa afe kutokana na maradhi yanayoweza kuepukwa.
Waziri Müller aliyasema hayo kwenye mkutano wa wafadhali wa kimataifa uliofanyika mjini Berlin ambapo washiriki walijadili mikakati ya kutoa chanjo za kuyakinga maradhi kama surua, kifaduro,homa ya manjano na maradhi ya kupooza.
Mkutano huo wa kile kinachofahamika kama mfungamano wa kimataifa wa chanjo dhidi ya maradhi yanayoweza kuepukwa Gavi, uliwaleta pamoja viongozi,kutoka nchi zinazoendelea na wafadhili kutoka duniani kote.
Tanzania yapata mafanikio
Akihutubia kwenye mkutano huo wa "Gavi" Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania aliarifu juu ya mafanikio ya nchi yake katika kutoa chanjo kutokana na msaada wa Gavi Amesema kutokana na msaada wa Gavi ,Tanzania imeweza kutoa chanjo mpya 11. Rais Kikwete amefahamisha kwamba Tanzania imo miongoni mwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara zinazotoa chanjo kwa mafanikio.
Rais Kikwete amesema asilimia 90 ya watoto nchini Tanzania wamechanjwa ili kukinga maradhi ya kupooza na asimilia 90 nyingine wamepewa chanjo ya kuuzuia ugonjwa wa surua.
Mpango unaokusudiwa kutekelezwa na asasi ya Gavi ni kutoa chanjo kwa watoto Milioni 300 katika nchi zinazoendelea hadi mwaka wa 2020.
Mfungamano wa Gavi ni ushirikiano baina ya Shirika la Afya Duniani,WHO,Benki ya Dunia, Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa na wafadhili kadhaa wa kimataifa ikiwa pamoja na Wakfu wa Bill Gates.
Kiasi cha fedha kinachohitajika ili kuweza kuendelea huduma ya chanjo ni Euro Bilioni 6.6 . Wakfu wa Bill Gates umechangia kiasi cha dola Bilioni 1.5. Gates amesema ndoto yake ni kuona kwamba kila mtoto anapata chanjo za kukinga maradhi. Ujerumani itachangia kiasi cha Euro Milioni mia sita.
Kutokana na mradi wa Gavi watoto nusu Bilioni wameshapatiwa chanjo dhidi ya maradhi kama kichomi na surua katika nchi zinazoendelea.
Mwandishi:Werkhäuser Nina
Tafsiri:Mtullya abdu.