1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala Ethiopia chamchagua kiongozi mpya

28 Machi 2018

Chama tawala nchini Ethiopia kimemchagua Abiye Ahmed kuwa mwenyekiti wake mpya, baada ya Hailemariam Desalegn kujiuzulu mwezi Februari. Kuchaguliwa katika nafasi hiyo kunamfanya Abiye kuwa waziri mkuu moja kwa moja.

https://p.dw.com/p/2v7Sx
Dr. Abiy Ahmed
Picha: DW/S. Teshome

Shirika utangazaji la umma EBC limeripoti kuwa bazara la muungano tawala wa Ethiopian People's Revolution Democratic Front (EPRDF) lenye wajumbe 180 lilimchaguwa Abiye kumrithi Hailemariam kama mwenyekiti wa muungano, hii ikimaanisha anakuwa waziri mkuu moja kwa moja.

"Katika kikao cha leo, baraza limepiga kura na kumchaguwa Abiye Ahmed kama mwenyekiti," alisema mtangazaji wa EBC bila kutoa ufafanuzi. Vyombo vya habari vinavyoelemea serikali vilisema Abiye alishinda asilimia 60 ya kura katika baraza hilo.

Abiye, anaetokea katika kabila la Oromo, atachukuwa jukumu la kuiongoza serikali ya taifa hilo la pili kwa kuwa na wakaazi wengi barani Afrika. Muungano tawala umepambana kudhibiti machafuko sugu na ya vurugu tangu 2015, ambaye yamegeuka kuwa changamoto yake kubwa zaidi tangu 1991.

Hailemariam alitangaza kujiuzulu mwezi uliopita kama juhudi za kurahisisha njia ya mageuzi. Hatua hiyo ilikuja baada ya migomo na maandamano karibu na mji mkuu kufanikisha kuachiwa kwa wanachama wa upinzani.

Äthiopien kündigt Freilassung politischer Gefangenen an | Hailemariam DesalegnDesalegn
Waziri mkuu aliejiuzulu Hailemariam Desalegn.Picha: picture alliance/AA/E. Hamid

Maandamano hayo ya kuipinga serikali yalianza 2015 kuhusiana na haki za umiliki wa ardhi kabla ya kupanuka na kugeuka maandamano ya kudai haki za kisiasa na kibinadamu.

Serikali imetangaza mara mbili utawala wa hali ya hatari, ya karibuni zaidi ikiw ani baada ya tangazo la kujiuzulu kwa Hailemariam, ili kufhibiti machafuko hasa katika mkoa wa Oromiya, ambao ndiyo wenye watu zaidi nchini humo. Makundi ya kutetea haki za binadamu yamesema kwamba wakati wa vurugu hizo, vikosi vya usalama vimeua mamia ya watu.

Changamoto zinazomkabili

Abiye anakabiliwa na changamoto ya kutekeleza mageuzi ya kidemokrasia ambayo serikali imeahidi kuyatekeleza. Pia ana jukumu la kuziba nyufa zilizojitokeza ndani ya chama tawala.

Wakati kura ya kuthibitisha hali ya pili ya hatari baada ya kujiuzulu kwa Hailemariam ilipokuja bungeni mapema mwezi huu, karibu wabunge 90 walipiga kura ya kupinga muswada huo licha ya kuwa wanachama wa muungano huo, hali iliodhihirisha mgawiko mkubwa ndani ya muungano huo.

"Anakabiliwa na jukumu la kupanua uwanja wa kisiasa na kujongeleana na upinzani. Pia anapaswa kujibu madai ya umma," amesema Asnake Kefale, profesa msaidizi wa somo la sayansi ya siasa katika chuku kikuu cha Addis Ababa. Uchaguzi wa bunge umepangwa kufanyika 2020.

Äthiopien Protesten der Oromo in Bishoftu
Waandamanaji wa Kiethiopia wakiimba nyimbo wakati wa sherehe ya watu wa Oromo katika mji wa Bishoftu, katika jimbo la Oromiya, katika picha hii ya maktaba iliyopigwa Oktoba 2, 2016. Picha: REUTERS/File Photo/T. Negeri

Matumaini ya kupungua mgogoro wa kikabila

Wachambuzi wanasema kuchaguliwa kwa mtu wa kabila la Oromo katika nafasi yeyen nguvu zaidi kisiasa nchini humo kunaweza kutuliza wasiwasi. Kabila la Oromo linachangia asilimia 34 ya wakaazi milioni 100 wa Ethiopia, lakini hawajawahi kushika madaraka katika historia ya sasa ya taifa hilo.

Pamoja na kundi jengine kubwa zaidi la kikabila la Amhara, wameongoza maandamano ya mitaani dhidi ya serikali tangu 2015. Abiye ndiye mwenyekiti wa chama cha Oromo People's Democratic Party, mmoja ya vyama vinne vya kikabila vilivyomo ndani ya muungano wa EPRDF.

Anazungumza lugha tatu za Kiethiopia, ana shahada ya uzamivu katika amani na usalama kutoka chuo kikuu cha Addis Abab na alihudumu katika jeshi. Pia alihudumu kwa muda mfupi kama waziri wa sayansi na teknolojia katika baraza la Hailemariam.

Baadhi ya wachambuzi na wanasiasa wa upinzani wamelaumu kuongezeka kwa mizozo ya kikabila katika taifa hilo lenye makabila mengi kwa mfumo wa majimbo wa Ethiopia, ambao ulichora tena mipaka ya majimbo kwa sehemu kubwa kwa misingi ya kikabila mwaka 1991.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Josephat Charo.