1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala cha Tanzania chaanza vikao vya awali

31 Machi 2022

Chama tawala nchini Tanzania CCM, leo kimeanza vikao vyake muhimu kuelekea katika mkutano mkuu maalumu utakaofanyika kesho Ijumaa mjini Dodoma.

https://p.dw.com/p/49H04
Präsidentschaftskandidat der CCM in Sansibar: Dr.Ali Mohamed Shein
Picha: DW

Vikao hivyo vya leo vitatoa dira halisi kuhusu mkutano ambao pamoja na mambo mengine utaidhinisha marekebisho ya katiba ya chama hicho.

Baadhi ya mambo ambayo yanatarajiwa kuwekwa sawa na Kamati Kuu pamoja na Halmashauri yake ni pamoja kupanga mtiririko wa matukio yatakayozingatiwa na wajumbe wa mkutano huo unaofanyika wakati Rais Samia Suluhu akitimiza miezi 11 tangu achaguliwe kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Je huu ni mwanzo wa mabadiliko ya kikatiba?

Tansania Wahlen 2010
Wafuwasi wa CCM nchini TanzaniaPicha: AP

Suala la mabadiliko ya katiba ya chama hicho kilichoasisiwa tangu mwaka 1977 kwa kuunganisha vyama vya Tanu na ASP, ni ajenda kuu inayotawala mkutano huu ambao unafanyika kukiwa kumesaliwa na miezi sita kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu wa taifa ndani ya chama.

Marekebisho yanayotupiwa macho ni yale yaliyofanywa wakati wa uongozi wa hayati Rais John Magufuli aliyewaondoa makatibu wakuu wa mikoa kuingia katika vikao vya Halmashairi kuu kwa kile kilichoelezwa kupunguza gharama.

Chama hiki tawala kimekuwa na desturi ya kijitathmini kila baada ya uchaguzi mkuu na baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema mabadiliko haya ya katiba ni sehemu ya mkakati wa chama hicho kujaribu kuzikabili changamoto za wakati huu.

Azma ya kwenda na kasi ya kisiasa ya wakati huu.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka anasema mabadiliko hayo ya katiba yataiwezesha CCM kwenda na kasi ya wakati huu.

Marekebisho hayo ya katiba ya chama hicho tawala yanakuja wakati kukiwa na matumaini mapya kuhusu hali ya kisiasa ya nchi ambako inaaminika kuwa huenda marufuku vyama vya siasa kuendelea na mikutano ikiondolewa. Je kwa mabadiliko haya, CCM bado itaendelea kuwa na ushawishi ndani wapiga kura wake na hata kwa wale wasiopenda kuegemea upande wowote wa kisiasa? Eric Bernard ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa.

Kukamilika kwa mabadiliko ya katiba kwa chama hicho kunafungua njia kuanza mchaka mchaka wa uchaguzi wa ndani ya chama ambao utakaonza keshokutwa Jumamosi na kuendelea hadi Disemba kutakapofanyika uchaguzi mkuu wa chama.