1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha New Democracy chaongoza uchaguzi wa Ugiriki

18 Juni 2012

Chama cha New Democracy nchini Ugiriki kipo kwenye harakati za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kuutekeleza mpango wa kubana matumizi wa Umoja wa Ulaya utakaoiwezesha kujinasua kwenye mzozo wa uchumi unaokabili.

https://p.dw.com/p/15Gw4
Leader of conservative New Democracy party Antonis Samaras is cheered by supporters after his statement on the election results in Athens June 17, 2012. Samaras claimed victory in Sunday's national election, saying Greeks had voted to stay in the euro single currency. REUTERS/John Kolesidis (GREECE - Tags: POLITICS ELECTIONS BUSINESS TPX IMAGES OF THE DAY)
Parlamentswahl Griechenland Antonis SamarasPicha: Reuters

"Wagiriki leo wamepiga kura na kuamua nchi yao ibakie katika kanda ya sarafu ya Euro, wamechagua sera ambazo zitawaletea ajira, ukuaji wa maendeleo, haki na usalama" ni kauli ya kiongozi wa chama hicho Antonis Samara baada ya kupata ushindi kwenye uchaguzi wa jana.

Asilimia 74 ya kura zimeshahesabiwa hadi sasa na matokeo yanaonyesha chama cha New Democracy kimepata asilimia 30 ya kura zote, kikiwa mbele ya kile chenye msimamo wa mrengo wa shoto Syriza kinachopinga mpango wa kubana matumizi wa Umoja wa Ulaya ambacho kimepata asilimia 26.5 huku Pasok kinachounga mkono mpango huo kikiwa na asilimia 12.5. Samara anasema huo ni ushindi wa umoja wa ulaya si wa Ugiriki pekee.

Kiongozi wa chama cha Syriza Alexis Tsipras alikubali kushindwa jioni ya Jumapili. Wakati matokeo rasmi yanaonyesha hakuna chama kilichopata ushindi wa kutosha kuunda serikali peke katika viti 300 vya ubunge kama ilivyokuwa kwa uchaguzi wa Mei 6 mwaka huu, New Democracy na Pasok vina wingi wa viti vya kutosha kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Kwa utaratibu wa nchi hiyo, mshindi wa kwanza anapata ziada ya viti 50 bungeni na haki ya kuunda serikali mpya. Na kama kikishindwa fursa hiyo inakwenda kwa mshindi wa pili.

Umoja wa Ulaya waupongeza ushindi huo

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso pamoja na Rais wa Umoja huo Herman Van Rompuy wameukaribisha ushindi huo wakisema wanatumai serikali itaundwa mara moja na kuiahidi nchi hiyo kuwa Umoja wa Ulaya uko pamoja nayo.

Jose Manuel Barroso, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya
Jose Manuel Barroso, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa UlayaPicha: Reuters

Katika tamko lao la pamoja kando ya mkutano wa nchi za G20 mjini Los Cabos, Mexico, viongozi hao wamesema kuwa wanaheshimu na kuunga mkono maamuzi ya wananchi wa Ugiriki na wanaelewe vizuri namna walivyojitolea kuuinua uchumi wa nchi yao kwa kuujenga upya na kuleta maendeleo.

Ugiriki haina budi kuutii mpango wa kubana bajeti

Kutokana na patashika iliyougubika uchaguzi huo, serikali yoyote itakayoundwa nchini humo haitakuwa na muda wa kutosha kutimiza mashari yote ya kubana matumizi. Rais wa bunge la Umoja wa Ulaya Martin Schulz ameonya kuwa serikali mpya ni lazima itatue mzozo wa uchumi unaoikabili nchi hiyo.

Mawaziri wa Fedha wa nchi za Umoja wa Ulaya
Mawaziri wa Fedha wa nchi za Umoja wa UlayaPicha: dapd

"Tunatakiwa kuisaidia Ugiriki iweze kusimama yenyewe kupitia mpango wa kukuza ajira na maendeleo. Baada ya hapo itaweza kutimiza majukumu yake yenyewe", alisema Schluz wa kutoka chama cha Social Democrat cha Ujerumani. Suala hili ndio kipaumbele cha Ujerumani, maana tutakuwa gizani kama Kanda ya Sarafu ya Euro na Umoja wa Ulaya vitavunjika", ameongeza Schluz.

Mjini Brussels Ubelgiji, mawaziri wa fedha wa kanda hiyo wameonya kuwa mpango wa kubana matumizi na mageuzi ya kiuchumi ndio njia pekee itakayoisaidia Ugiriki huku wakiahidi kuiunga mkono kwenye harakati zake za kusimama tena.

Mwandishi: Stumai George/DPAE

Mhariri: Hamidou Oummilkheir