1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIndia

Chama cha Modi hakitasimamisha wagombea Kashmir

Angela Mdungu
9 Mei 2024

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, katika kampeni za uchaguzi nchini humo kwa mara ya kwanza, tangu mwaka 1996, chama chake cha Bharatiya Janata hakitashiriki uchaguzi katika jimbo la Kashmir.

https://p.dw.com/p/4fg7v
Uchaguzi wa bunge India 2024
Waziri Mkuu wa India Narendra ModiPicha: Ajit Solanki/AP Photo/picture alliance

Eneo hilo limekuwa likipigania kujitawala kwa miaka 35 hali ambayo imeshasababisha vifo vya maelfu ya watu.

Chama cha Waziri Mkuu Modi, hakina uwakilishi katika uchaguzi kwenye jimbo hilo la Kashmir, badala yake vyama vya National Conference na chama cha demokrasia cha PDP ndivyo vinavyowania nafasi tatu za uwakilishi katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya Waislamu.

Vyama hivyo vitachuana ingawa vyote vinakiri kuwa vinakipinga chama cha Modi na vitaungana na chama cha Congress kinachoongozwa na Muungano wa upinzani.

Soma zaidi: Indian yarejea kwenye uchaguzi katikati ya kitisho cha joto

Wachambuzi na vyama vya upinzani wanasema kuwa chama cha Bharatiya Janata (BPJ) kiliamua kukwepa kushiriki uchaguzi huu kwa sababu matokeo yanaweza kusababisha mkanganyiko kwa dhana ya waziri Mkuu Modi ya kuwa na Kashmir yenye amani na ujumuishwaji tangu alipoiondolea hadhi maalumu mwaka 2019 na kuiweka chini ya udhibiti wa  New Delhi.

Chama cha BJP, pamoja na washirika wake vinashiriki katika uchaguzi kwenye maeneo mengine yote ya India na kinatarajiwa kushinda viti vingi katika bunge lenye viti 543.

Modi anasema uamuzi wake wa mwaka 2019 umerejesha hali kuwa ya kawaida Kashmir baada ya miongo mingi ya umwagaji damu. Anasema pia muda si mrefu ataanzisha uwekezaji na kutengeneza nafasi za ajira katika jimbo hilo.

Soma zaidi: Modi aapa kuongeza matumizi ya kijamii na kuifanya India kuwa kitovu cha uzalishaji

Waziri wa mambo ya ndani wa India Amit Shah anaitetea serikali yake kwa kudai kuwa sasa, vijana wanashika kompyuta badala ya mawe waliyokuwa wakiyatumia kuwarushia maafisa wa usalama.

Kama sehemu ya hatua hiyo, jimbo la Jammu na Kashmir liligawanywa katika maeneo mawili yaliyo chini ya utawala wa serikali kuu. Eneo moja ni bonde la Kashmir lenye Waislamu wengi na eneo la pili ni la tambarare la Jamu lenye wahindu na milima ya Ladakh yenye wafuasi wa Budha.

Wakaazi wa Kashmir bado wanahisi kutengwa

Mahojiano yaliyofanywa na baadhi ya wakaazi, viongozi wa kisiasa, maafisa wa usalama na wachambuzi huko Kashmir na New Delhi yanaashiria kuwa, hali ya kutoridhika na kutengwa inaendelea kufukuta kwenye maeneo  ya Himalaya yenye ulinzi mkali.

Kwa miongo mingi, wakaazi na makundi ya wanaharakati wa haki za binadamu wamekuwa wakituhumu vikosi vya ulinzi vya India kwa kufanya ukatili dhidi ya Waislamu ambao ndiyo wengi. Serikali inasema visa vya unyanyasaji ni visa vinavyofanywa na mtu mmoja mmoja na kwamba inamshtaki mwanajeshi yeyote atakayekutwa na hatia ya kukiuka haki za binadamu.

Uchaguzi wa bunge India
Mashini ya kielektroniki ya kupigia kura ikisafirishwa kwa punda India Picha: Channi Anand/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo Profesa Sheikh Showkat Hussain, mtaalamu mstaafu wa sheria anasema chama cha Modi cha Bharatiya Janata  kilipaswa kuchukulia uchaguzi wa sasa kama kura ya maoni ambayo ingewanufaisha, lakini chama hicho kinaogopa.

Itakumbukwa kuwa katika uchaguzi mkuu wa Mei 2019, chama hicho kiliwania viti vitatu Kashmir na kilivipoteza vyote baada ya chama cha National Conference kupata ushindi. Mwaka 2022, tume iliyoteuliwa na serikali kuu ilibadilisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi ndani ya Kashmir na Jammu.

Soma zaidi: Kwanini India inazozana na Pakistan juu ya mkataba wa kihistoria?

Kiongozi wa chama cha National conference na Waziri wa zamani wa jimbo la Jammu na Kashmir Omar Abdullah anadai kuwa kubadilishwa huko kwa mipaka huenda kungekinufaisha chama cha Modi, lakini hakijaweka mgombea. Kwake hii inaashiria kuwa hali si hali ndani ya  Bharatiya Janata

Hata hivyo mkuu wa tawi la chama hicho ndani ya Kashmir Ravinder Raina anasema kuwa, kubadilishwa kwa mipaka kumeyapa maeneo ya Kashmir uwakilishi zaidi. Ameongeza kuwa kutokushiriki kwa chama chake katika uchaguzi huu ni sehemu ya mkakati mpana, ambao hata hivyo hakuutolea maelezo zaidi.