Chama cha CDU chashinda uchaguzi wa North Rhine Westphalia
15 Mei 2017Matokeo ya awali yanaonyesha CDU imeshinda uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili kwa asilimia 33 huku SPD ambacho kimeliongoza jimbo hilo kwa karibu nusu karne kikiibuka katika nafasi ya pili kwa asilimia 31.3 na chama cha Free Democratic Party FDP kinachonuia kurejea katika bunge la Shirikisho la Ujerumani kikiwa katika nafasi ya tatu kwa asilimia 12.5 ya kura.
Ushindi huo wa CDU umepiga jeki matumaini ya Merkel kusalia madarakani kwa muhula wa nne katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwezi Septemba mwaka huu. Mgombea Ukansela wa SPD Martin Schulz amesema matokeo hayo ni pigo kubwa kwa chama chake na kwake binafsi. Kupitia ukurasa wake wa Twitter Schulz amesema wameshindwa vibaya katika jimbo analotokea.
Schulz ashindwa nyumbani
Mgombea wa CDU Armin Laschet ambaye ni waziri mkuu mtarajiwa wa North Rhine Westphalia amesema ni siku muhimu kwa jimbo hilo baada ya ushindi wa jana akiongeza wamefanikiwa kufikia malengo yao mawili kuushinda muungano wa SPD na chama cha walinda mazingira cha kijani na pia kuwa chama imara zaidi katika jimbo hilo.
Kufuatia matokeo hayo, waziri mkuu wa NRW Hannelore Kraft amejiuzulu kama kiongozi wa SPD katika jimbo hilo na kusema anawajibika kikamilifu kwa matokeo mabaya kwa chama chake akiongeza walifanya kila wawezalo kulisogeza mbele jimbo hilo lakini yaonekana juhudi zao hazikutosha na hawakuweza kupata ridhaa ya wapiga kura.
Maafisa wa uchaguzi wa jimbo hilo la North Rhine Westphalia wamesema idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa kubwa ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita. Asilimia 65. 2 walishiriki uchaguzi huo.
Ushindi wampa matumaini Merkel
Zaidi ya watu milioni 13 wakaazi wa jimbo hilo walisajiliwa kama wapiga kura hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi ya wapiga kura waliosajiliwa kuliko katika jimbo lolote lingine Ujerumani. CDU imeonekana kunufaika kutokana na ghadhabu ya wapiga kura kuhusu usalama, kuongezeka kwa uhalifu, elimu, uhamiaji na idadi ya wasio na ajira.
SPD imeliongoza jimbo la North Rhine Westphalia kwa miaka 46 kati ya miaka 51 iliyopita. CDU ililiongoza tu kwa miaka mitano kati ya mwaka 2005 hadi 2010.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Alternative für Deutschland AfD kilichopata asilimia 7.4 ya kura kwa mara ya kwanza kitaingia katika bunge la jimbo hilo hiyo ikimaanisha chama hicho kitakuwa na uwakilishi katika majimbo 13 kati ya 16 ya Ujerumani.
CDU inatumai kushinda katika uchaguzi mkuu chini ya uongozi wa Merkel ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2005 akisifiwa kwa kuifanya Ujerumani thabiti kisiasa, kiuchumi na katika safu ya kimataifa.
Mwandishi: Caro Robi/dpa/Dw English
Mhariri: Daniel Gakuba