1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Macron chashinda viti vingi bungeni

19 Juni 2017

Chama cha mrengo wa kati cha rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kilipata ushindi Jumatatu unaokipatia idadi kubwa ya wajumbe bungeni, jambo linalochora upya ramani ya siasa za Ufaransa.

https://p.dw.com/p/2evKV
Frankreich Parlamentswahlen Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/C. Archambault

Ushindi huo unampatia kiongozi huyo mchanga mamlaka ya kutekeleza mabadiliko yatakayovutia biashara. Ingawa hakikupata ushindi wa kupindukia kama ilivyotabiriwa, chama hicho cha Republic on the Move na washirika wake kilishinda viti 350 katika bunge hilo lenye viti 577, baada ya duru ya pili ya upigaji kura iliyoshuhudia majina makubwa kutochaguliwa.

Chama hicho alichokibuni Macron miezi 14 tu iliyopita kimezusha taharuki ya kisiasa hata ingawa ushindi wake haukufikia ule wa viti 470 uliokuwa umetabiriwa na kura za maoni.

Ushindi huo unampatia Macron mwenye umri wa miaka 39, mojawapo ya ushindi mkubwa tangu vita vya pili vya dunia, na mwandishi Alexis Brezet katika gazeti linaloegemea mrengo wa kulia Le Figaro aliuita ushindi wake kama mabadiliko, "katika historia ya taasisi zetu, ni mabadiliko yasiyo na kifani tangu mwaka 1958," aliandika Brezet.

Wachambuzi wanasema Macron anastahili kuwasikiliza raia

Ushindi huo utampatia Macron uhuru wa kuendeleza ajenda yake ya kulegeza sheria za kazi ili kujaribu kuongeza kiwango cha ajira na kuleta mwamko mpya wa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya. Lakini Nicolas Sauger ambaye ni Profesa wa masuala ya Ulaya alisema Macron ni sharti awasikilize raia wa Ufaransa kwa kuwa ni asilimia 30 tu ya wapiga kura waliokuwa wana imani kuwa chama chake kitashinda idadi kubwa ya viti bungeni.

Die vorsitzende der Partei «La Republique en Marche» Catherine Barbaroux
Kiongozi wa chama cha REM chake Macron Catherine BarbarouxPicha: Picture alliance/dpa/F. Mori/AP

"Tatizo tulilo nalo sasa ni kuubadilisha mtazamo wa raia tangu ile duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais wa utawala uliopo," alisema Sauger, "mtazamo huu haubadiliki hata kwa kuwasili kwa Macron. Raia wa Ufaransa wanaonekana hawamuamini kuweza kutatua matatizo yote. Kwa hiyo uaminifu wa raia kwa Macron ni mchache."

Wapinzani wake walisema Macron hana uungwaji mkono mkubwa kutokana na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza huku kiongozi wa mrengo wa kushoto Jean-Luc Melenchon akisema Wafaransa kwa sasa wako katika mgomo.

Marine Le Pen aingia bungeni kwa mara ya kwanza

Msemaji wa serikali Christophe Castaner alisema hatua ya zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura kuamua kusalia nyumbani badala ya kushiriki zoezi hilo ni ishara ya jinsi siasa za Ufaransa zinavyostahili mabadiliko.

Parlamentswahl in Frankreich 2017 Marine Le Pen Front National
Marine Le Pen ameingia bungeni kwa mara ya kwanzaPicha: Getty Images/AFP/F. Lo Presti

Wakati huo huo Marine Le Pen wa chama cha mrengo wa kulia cha National Front aliyeshindwa na Macron katika uchaguzi wa rais Mei 7, alifanikiwa kuingia bungeni kwa mara ya kwanza katika taaluma yake ya siasa ingawa chama chake kilipata viti 8 tu kinyume na lengo lake la viti 15.

Wakaazi wa eneo la Henin-Beaumont, eneo ambalo Le Pen alishinda kiti chake walikuwa na maoni mseto.

"Nimevunjika moyo, nimevunjika moyo kabisa wa kuishi hapa na kwa kweli nafikiri nitaondoka eneo hili. Sitoweza kuishi katika sehemu iliyojaa watu wa mrengo wa kulia," alisema Noredine Khial.

Jean Pierre Poupeau ni mkaazi mwengine na yeye alisema anataraji kwamba Le Pen atakuwa anampinga Macron kutekeleza baadhi ya mambo aliyoyapendekeza kama kubadili sheria za kazi na kuwatoza ushuru wazee kwani ni aibu.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo