1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Le Pen chazindua kampeni uchaguzi Bunge la Ulaya

4 Machi 2024

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha nchini Ufaransa cha mwanasiasa kigogo Marine Le Pen kimezindua kampeni yake ya kuwania viti vya Bunge la Ulaya.

https://p.dw.com/p/4d7rD
Viongozi wa chama cha Rassemblement National wakiongozwa na Marine Le pen (katikati).
Viongozi wa chama cha Rassemblement National wakiongozwa na Marine Le pen (katikati). Picha: Bourguet Philippe/BePress/ABACA/picture alliance

Chama hicho kimesema uchaguzi huo wa mwezi Juni utakuwa kura ya maoni kuhusu suala la "Uhamiaji".

Uchunguzi wa maoni ya umma unaonesha chama hicho cha Rassemblement National kitapata mafanikio makubwa yanayofikia asilimia 28 hadi 30 ya kura, matokeo yatakayotoa changamoto isiyo mfano kwa vyama vilivyozoeleka nchini Ufaransa ikiwemo cha Rais Emmanuel Macron.

Rais wa chama hicho cha Bibi Le Pen, Jordan Bardella, ambaye ndiye atakiongoza kwenye uchaguzi huo wa Bunge la Ulaya, amesema uchaguzi unaokuja utakuwa kipimo cha kauli ya umma wa Ufaransa unaoelemewa na mzigo wa wahamiaji.

Matamshi hayo ameyatoa alipohutubia mkutano wa kwanza wa kampeni kwenye mji wa kusini mwa Ufaransa wa Marseille. Uchaguzi wa bunge la Ulaya utafanyika tarehe 9 Juni na suala la uhamiaji linatazamiwa kuwa moja ya ajenda za kipaumbele.