1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha kizalendo chaongoza matokeo ya uchaguzi Uswisi

Josephat Charo
23 Oktoba 2023

Chama cha SVP kilifanya kampeni kikijikita juu ya mada iliyopendwa sana ya mapambano dhidi ya uhamiaji mkubwa na uwezekano wa umma wa Uswisi kufikia milioni 10.

https://p.dw.com/p/4Xsqa
Schweiz | SVP Wahlplakat zur Parlamentswahl
Mwendesha baiskeli akipita bango la uchaguzi la wagombea wa chama cha SVP, 17.10.2023Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Chama cha kizalendo cha siasa za mrengo wa kulia Swiss People's Party, SVP, ambacho kilifanya kampeni dhidi ya uhamiaji mkubwa, kimeongoza kirahisi katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana Jumapili nchini Uswisi. Kwa mujibu wa matokeo ya awali baada ya zaidi ya nusu ya kura kuhesabiwa, chama hicho kimejikingia asilimia 29 ya kura katika uchaguzi wa bunge, kikiimarisha wingi wake bungeni kwa zaidi ya asilimia tatu.

Rais wa chama cha SVP, Marco Chiesa amekiambia kituo cha kitaifa cha televisheni RTS kwamba wamepewa mamlaka ya wazi na umma wa Uswisi kuwasilisha masuala yanayowahusu kama vile uhamiaji usio halali. Chama cha siasa za mrengo wa kushoto cha Social Democratic kinafuata katika nafasi ya pili na asilimia 18 ya kura, kikifuatiwa katika nafasi ya tatu na chama cha siasa za wastani zinazoegemea mrengo wa kulia, The Centre.