UN na Marekani watoa mwito uchaguzi ufanyike Sudan Kusini
8 Machi 2022Umoja wa Mataifa na Marekani zimewatolea mwito viongozi wa Sudan Kusini kufanya juhudi zaidi kuandaa chaguzi ambazo zimepangwa kufanyika katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja au kusababisha hatari ya kutokea janga.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Sudan Kusini Nicholas Hayson ameliambia baraza la usalama la Umoja huo kwamba chaguzi za nchi hiyo zina uwezekano wa kuleta mwamko wa kuijenga nchi au kusababisha janga.
Kwa mtazamo wake ni kwamba kwa kiasi kikubwa hali inategemea nia ya kisiasa na uongozi wa Sudan Kusini kufanya kazi pamoja.Na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataida Linda Thomas Greenfield amesema ili kufanya kazi kuelekea demokrasi ya kweli,serikali ya Sudan Kusini itapaswa kuchukua hatua za wazi za kutekeleza vipengele vilivyobainishwa katika mkataba uliofikiwa wa kuimarisha mchakato wa amani.
Kwa maneno mengine inatakiwa uwepo mchakato wa kuandika katiba utakaozijumuisha pande zozte,yafanyike mabadiliko ya usimamizi wa fedha za umma.mpangilio wa kiusalama wa kipindi cha mpito pamoja na kuwepo mfumo wa mpito wa kusimamia sheria.
Msimamo wa Marekani
Ingawa kwa bahati mbaya sana balozi huyo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema serikali ya Sudan Kusini iko nyuma mno kufikia mambo muhimu yaliyofikiwa kuelekea kufanyika uchaguzi,mambo yaliyowekwa wazi katika makubaliano.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa March 15 kutowa uamuzi kuhusu kurefusha kipindi cha kubakisha kikosi cha kulinda amani nchini humo kwa mwaka mmoja ambacho ni moja ya ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa wenye gharama kubwa zaidi katika historia ya Umoja huo,zikitumika zaidi ya bilioni 1 kwa mwaka. Hayson ametowa rai ya Ujumbe huo kuendelea kujumuisha kiwango cha sasa cha wanajeshi 17,000 na askari polisi 2,100.
Tahadhari ya UN
Umoja wa Mataifa ulikwisha tahadharisha mnamo mwezi Februari kwamba wakati nchi hiyo ina kipindi cha chini ya mwaka mmoja mpaka kufikia uchaguzi,kuna hatari Sudan Kusini ambayo ilipata uhuru wake mwaka 2011 ikatumbukia kwenye vita.
Kati ya mwaka 2013 na 2018 Sudan Kusini ilishatumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyohusisha upande wa Riek Machar na upande wa pili rais Salva Kiir na kiasi watu 400,000 waliuwawa na mamilioni waliachwa bila makaazi.
Makubaliano ya amani yaliyotiwa saini 2018 ndiyo yaliyoleta serikali ya umoja wa kitaifa ya kugawana madaraka na kuapishwa Februari mwaka 2020 ambapo Kiir alichukuwa urais na Machar akawa makamu wake. Lakini vipengele kadhaa vya makubaliano ya amani kwa kiasi kikubwa havijaweza kutekelezwa mpaka sasa,sababu kubwa hasa ni mivutano isiyokwisha kati ya pande hizo mbili zenye uhasama.