1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA yaanza mchujo wa wagombea ubunge na udiwani

George Njogopa13 Julai 2020

Chama kikuu cha upinzani Tanzania, Chadema kinaanza rasmi mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kuwachuja wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani.

https://p.dw.com/p/3fE5R
Tansania John Mnyika Generalsekretär Oppositionspartei CHADEMA
Picha: DW/Said Khamis

Chama hicho kinaanza mchakato huo huku wasiwasi ukiongezeka namna kitakavyofanikiwa kuvuka katika hatua hiyo hasa baada ya kushuhudiwa idadi kubwa ya wagombea wakijitokeza katika baadhi ya majimbo. Wagombea wote wanaanza kumulikwa na wapiga kura katika maeneo yao ya majimbo kwa kipindi cha siku tatu kuanzia Jumatatu(13.07.2020) na baadaye vikao vya chama vitaaanza kuwajadili. Baada ya mchujo huo kukamilika katika ngazi ya majimbo, majina ya wagombea wote yanatarajiwa kupelekwa na kujadiliwa na kamati kuu ya chama hicho.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho, Reginald Munisi anasema kuwa kura hizo za maoni zinafanyika kwa ajili ya kupata picha halisi kabla ya vikao vya chama ngazi ya juu havijaanza kukutana mwishoni mwa mwezi huu kwa kupata majina ya wagombea wote nchi nzima.

Kumekuwa na idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza wakiwania nafasi za ubunge na udiwani, na chama hicho kitapaswa kuchanga vyema karata zake namna ya kuwapata wagombea hao hasa katika kanda ya kaskazini inayotajwa kuwavutia watia nia wengi.

Tansania | Politische Partei | CHADEMA
Meya wa zamani wa Ubungo Boniface Jacob akikabidhiwa fomu ya kuwania ubungePicha: DW/S. Khamis

Kanda hiyo inayojumuisha mikoa kama Arusha na Kilimanjaro ina jumla ya wagombea zaidi ya 56 waliojitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama. Hali hiyo inatajwa pia kujitokeza katika kanda nyingine kama ile ya Nyasa inayodaiwa kuwa na wagombea wengi kuliko kanda nyingine zozote.

Kuwepo kwa idadi kubwa ya wagombea kunazua maswali mengi namna chama hicho kitakavyofanikiwa kuvuka daraja hilo bila kuwepo kwa mtikisiko wowote ndani ya chama.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, ameondoa uwezekano wa chama hicho kukumbwa na mkwamo wa kisiasa. Anasema uwepo wa idadi kubwa ya wagombea ni ishara ya namna chama hicho kinavyoendelea kukubalika katika nchi.

Kwa hatua hiyo chadema kinakuwa chama cha kwanza kuanzisha mchakato wa kuwachuja wagombea wake wa ubunge, wakati vyama vingine vikiendelea kujipanga kuelekea katika uchaguzi huo wa Oktoba

George Njogopa, DW-Dar es salaam