Chadema yaaanza kuwahoji wabunge walokiuka msimamo wa chama
27 Novemba 2020Hayo yanajiri mnamo wakati kuna shinikizo kubwa kutoka kwa wafuasi wa chama hicho ikiwamo makundi ya wanawake wanaotaka wabunge hao watimuliwe kutoka kwenye chama.
Kyenye ujumbe wa aina mbalimbali wafuasi wa chama hicho vijana kwa wanawake wanatuma ujumbe kwa kamati kuu inayokutana kwa dharura eneo la Bahari Beach kuwahoji na kisha kuwajadili wabunge hao.
Wanachama hao ambao nyakati za asubuhi walikusanyika katika makao makuu ya chama hicho eneo la Kindondoni, wanataka kamati kuu isipepese macho wakati ikiwajadili wabunge hao na wanasisitiza kuwa kuwaondolea uanachama wao ndiyo suluhu ya kikinusuru chama hicho.
Ni mpasuko au mvurugano ndani ya chama?
Maoni ya wanachama hao yanazidi kukoleza mwito uliotolewa na mabaraza ya wanawake kutoka wilaya mbaliambali waliotoa tamko kutaka wabunge hao wawekwe kando ndani ya chama hicho.
Mbali ya wanawake kujitokeza hadharani kuweka msimamo wao kadhalika makundi ya vijana nayo pia yanaonekana kuchukua msimamo wa iana hiyo hiyo.
Baadhi ya vijana hao waliojitokeza kwenye ofisi za chama hicho walionekana wakiwa na mabango mengine yakiwa na ujumbe ulioandikwa Covid 19.
Katika eneo la Bahari Beach nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, wajumbe wa kamati kuu wamejifungia wakiendelea na mkutano wa kuwahoji wabunge hao ambao wanadaiwa kwenda kinyume na msimamo wa chama.
Kikao hicho ambacho kinatupiwa macho na wengi ndicho kitakachoamua hatma ya wabunge hao kuendelea kusalia ndani ya chama au la.
Je wabunge hao watavuliwa uanachama?
Duru za habari zinasema kwamba kuna uwezekano huenda wabunge hao wakavuliwa uanachama hatua ambayo inaweza pia ikaanzisha mvutano mwingine wa pande zinazo waunga mkono na wale wanapendelea kuona wanawekwa kando.
Wikii iliyopita wanachama hao walionekana katika viwanja vya bunge wakila kiapo cha kuwa wabunge wa viti maalumu ilihali chama chao kikiwakana kwa kusema hakikupeleka majina yao kwenye tume ya taifa ya uchaguzi.
Chadema pamoja na vyama vingine vya upinzani vimeweka msimamo wa pamoja kushinikiza kuitishwa kwa uchaguzi mwingine kwa madai uchaguzi wa Oktoba 28 ulitawaliwa na vitendo vya udanganyifu.