1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHADEMA kufanya kampeni katika ngome za CCM

14 Septemba 2020

Chama kikuu cha upinzani Tanzania Chadema kimesema pamoja na baadhi ya majimbo wagombea wa ubunge wa chama tawala CCM kupita bila kupigwa, bado kitafanya kampeni katika maeneo hayo

https://p.dw.com/p/3iSE6
Tansania Tundu Lissu Präsidentschaftskandidat
Picha: DW/S. Khamis

Hayo yanakuja wakati vyama vyote vikiendelea kukutana na wapiga kura katika hatua muhimu ya kuzinadi sera zao kuelekea katika uchaguzi wa Oktoba 28. 

Chama hicho ambacho mgombea wake wa urais, Tundu Lissu yuko mkoani Iringa akiendelea kujiuza kwa wananchi, kimesema licha ya kuwa hatma ya wagombea wake 20 bado haijajulikana kutokana na rufaa zao kuchelewa kutolewa maamuzi, kinaamini kina nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika uchaguzi wa mwaka huu. Soma pia: NEC yashughulikia pingamizi 100 kati ya 500

Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika amewaambia waandishi wa habari kuwa tathmini ya chama hicho kuhusiana na wabunge walioko majimboni inaonyesha wamekuwa wakipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wapiga kura, ishara ambayo amedai kuwa ni dalili njema kuelekea katika tarehe ya uchaguzi.

Tansania Dodoma VEröffentlichung Parteiprogramm der CCM | John Magufuli
Kiongozi wa CCM Rais Magufuli apeleka kampeni ChatoPicha: DW/E. Boniphace

Mwanasiasa huyo aliyekuwa bungeni kwa miaka 10, amesema ingawa katika baadhi ya majimbo wagombea wa ccm wanatajwa kupita bila kupingwa, hilo halimaanisha kwamba chama hicho kitayakwepa majimbo hayo kuendesha kampeni zake. Soma pia: Tanzania yaihakikishia Marekani uchaguzi utakuwa huru

Naye mgombea wa chama tawala CCM, Rais John Magufuli leo amerejea tena kwenye majukwaa ya kampeni baada ya kujipa mapumiziko ya siku tatu, akianza ungwe hii ya pili katika jimbo lake la uchaguzi la Chato, mkoani Geita.

Kiongozi huyo anayewania muhula wa pili amewashangaa wapinzani wanaokosoa sera zake akisema anaamini hakuna hata mmoja kati ya waliojitokeza anayeweza kufikia robo ya utendaji wake wa miaka mitano. Soma pia: Maaskofu wataka uchaguzi wa huru na haki Tanzania

Wagombea wengine ikiwamo mwenyekiti wa chama cha Cuf Profesa Ibrahim Lipumba anayewania nafasi hiyo kwa mara ya tano anasema uongozi wa chama tawala umerudisha nyuma ustawi wa maisha ya watanzania wengi.

Wagombea wote mbali ya kuendelea kutegemea vyombo vya habari vya kawaida kufikisha ujumbe wao, lakini pia wanaegemea zaidi mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuwafikia wapiga kura wao.

Baadhi ya mitandao hiyo ni ile inayomilikiwa na vyama vyenyewe na uamuzi huo huenda pia unachangiwa na wasiwasi pengine hoja zao za ukosoaji kwa mamlaka zisipeperushwe moja kwa moja na vyombo hivyo.

George Njogopa, DW Dar es Salaam