CDU yashinda kwa kishindo uchaguzi wa jimbo la NRW-Ujerumani
16 Mei 2022Chama cha Christian Democratic Union kimenyakua ushindi katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine-Westphalia hapa Ujerumani. Matokeo rasmi ya awali yameonesha chama cha Social Democratic SPD kimepata pigo kubwa katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili.
Matokeo ya uchaguzi wa Jumapili katika jimbo hili la wakaazi wengi zaidi nchini Ujerumani la NRW yametangazwa leo asubuhi na chama cha Christian Democratic Union CDU kikiongozwa na Hendrik Wüst kimeibuka na ushindi mkubwa kikijipatia asilimia 35.7 ya kura. Punde baada ya kutangazwa matokeo hayo,katika kambi ya chama hicho, Wust ambaye pia ni waziri kiongozi wa sasa katika jimbo hili alikuwa na haya ya kusema.
''Wananchi wametupa ushindi mkubwa wa wazi na mamlaka ya kuunda na kuongoza serikali ijayo''
Chama cha Social Democratic kilijinyakulia asilimia 26.7 wakati washirika wake katika serikali kuu,chama cha kijani kilijipatia asilimia 18.2 na FDP kimeondoka na asilimia 5.9. Chama cha siasa kali kinachopinga wageni cha AfD kilipata asilimia 5.4 na kuvuka kiunzi kinachotakiwa kubakia katika bunge la jimbo hilo mjini Dusseldorf.
Chama cha kushoto Die Linke kimeshindwa kuingia bungeni kwa mara nyingine baada ya kujikingia asilimia 2.1 pekee ya wapiga kura. Hata hivyo pia idadi ya waliojitokeza kupiga kura ya asilimia 55.5 ni ndogo sana kiasi ambacho hakijawahi kuonekana katika historia ya uchaguzi wa jimbo hili.
Ama kwa upande wa chama cha SPD wameshindwa kwa mara ya pili safari hii ndani ya kipindi cha wiki mbili ambapo katika uchaguzi wa jimbo la Schleswig-Holstein pia walishindwa na CDU mwanzoni mwa mwezi huu, na matokeo waliyopata NRW ndiyo matokeo yake mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika uchaguzi wa jimbo hilo katika historia yake ya miaka 76.
Chama cha kijani kimejiongezea umaarufu ikilinganishwa na uchaguzi wa jimbo hilo 2017. Kwa maana hiyo sasa chama hicho cha Kijani ndicho kitakachokuwa na usemi mkubwa wa kuamua nani ataongoza serikali ya jimbo la NRW.
Hivi sasa jimbo hilo linaongozwa na serikali ya muungano kati ya vyama vya CDU na FDP lakini kwa matokeo ya uchaguzi wa Jumapili vyama hivyo vimepoteza wingi katika bunge la mjini Dusseldorf na hivyo kufungua nafasi ya kufanyika mazungumzo ya kutafuta muungano mpya.
Chama cha Kijani sasa ndicho chenye karata ya turufu, kina khiyari kuchagua kitakuwa tayari kuwa serikalini na CDU au SPD.Mgombea wa CDU Hendrik Wust ameshasema yuko tayari kuzungumza na vyama vyote isipokuwa AfD.
"Sasa nitakwenda kuzungumza na vyama vingine na nitafanya kila niwezalo kuhakikisha tunaondoka kwenye hali ngumu na kuongoza kwa kuaminika.Naamini kwamba nchi yetu itazikabili changamoto za baadae kwa uwezo wake wote''
Kiongozi wa SPD Kevin Kühnert,amesema muungano kati ya chama chao na Kijani bado una nafasi na hasa kwa kuzingatia kwamba wananchi wa jimbo hilo la NRW hawautaki muungano wa sasa kati ya CDU na FDP.