1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yasema Rais Magufuli kutoongeza muda madarakani

Deo Kaji Makomba
9 Februari 2021

Chama tawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzi, CCM kimesema wabunge wa nchi hiyo wana uhuru wa kutumia uhuru wa bunge kuzungumza maoni yao kuhusiana na kuongeza muda wa kukaa madarakani kwa rais wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3p7Zp
Tansania Amtseid des Präsidenten John Pombe Magufuli
Picha: Tanzania Presidential Press Service

Kauli hiyo ya CCM imetolewa jijini Dodoma na Katibu wake wa itikadi na Uenezi Humphrey Polepole wakati akimpa taarifa mbunge wa Jimbo la Konde, Zanzibar kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Khatib Said Haji, aliyeonyesha kukerwa na baadhi ya wabunge wa CCM mara kwa mara kutamka bungeni kuwa Rais John Magufuli anastahili kuongezewa muda wa kukaa madarakani.

Hata hivyo, Polepole amesema kinachozungumzwa bungeni hakiathiri msimamo wa chama CCM.

Mjadala wa ukomo wa rais Tanzania

Mjadala kuhusu ukomo wa rais kutawala Tanzania

Akichangia katika mjadala kuhusu mapendekezo ya mpango wa tatu wa maendeleo ya taifa wa miaka mitano pamoja na mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka 2021/2022, mbunge Said Haji, amesema kuwa tayari Rais Magufuli alikwishasema hataongeza muda wa kukaa madarakani, lakini cha ajabu baadhi ya wabunge wa CCM wamekuwa wakishadidia kiongozi huyo atakapomaliza muda wake wa uongozi aongezewe muda wa kuendelea kukaa madarakani.

Kauli ya mbunge huyo ilimfanya Polepole ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na Rais Magufuli, kutoa kauli bungeni kuhusiana na suala la Magufuli kuongezewa muda pindi atakapokuwa amemaliza muda wake wa uongozi.

Tansania Dar es Salaam  Chama Cha Mapinduzi CCM
Humphrey Polepole (kulia) akiwa na Vicent Mashinji, aliyekuwa Katibu Mkuu wa ChademaPicha: DW/Said Khamis

Polepole amesema kuwa Rais Magufuli hana mpango na wala hafikirii kuendelea kuwepo madarakani wakati kipindi chake cha uongozi kitakapokuwa kimemalizika.

Tangu alipoingia madarakani, Rais Magufuli katika awamu yake ya kwanza mwaka 2015, kuliibuka baadhi ya wabunge kutaka kiongozi huyo aongezewe muda pindi atakapomaliza kipindi chake cha uongozi na safari hii tena mbunge Festo Sanga wa Jimbo la Makete kupitia CCM alisisitiza kuhusu suala hilo, licha ya Rais Magufuli mara kwa mara kujitokeza hadharani kwa kusema kuwa ataendelea kuilinda katiba ya nchi ikiwa ni pamoja na kutoongeza muda wa kukaa madarakani.