1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yaanza mchakato wa kuwachuja watia nia wa ubunge

George Njogopa20 Julai 2020

Chama tawala nchini Tanzania CCM kimeanza mchakato wa kuwachuja wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kupitia kura za maoni zinazofanyika kote nchini. Idadi kubwa ya watia nia imejitokeza.

https://p.dw.com/p/3faal
Tansania Dar es Salaam  Chama Cha Mapinduzi CCM
Picha: DW/Said Khamis

Kuanzia siku ya Jumatatu (20.07.2020) na Jumanne zitakuwa siku muhimu kwa chama hicho kinapoanza hatua za mwanzo kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba. Wagombea wa nafasi zote wanajinadi kwa wapiga kura hatimaye wataamua hatma yao kutokana na matokeo yanayotarajiwa kuanza kufahamika jioni.

Kura hizi za maoni huenda zikawa moja ya mtihani mkubwa kwa chama hicho na jambo hilo linadhihirika kutokana na wingi mkubwa wa wagombea waliojitokeza kuwania nafasi za kuchaguliwa. Mbali ya wabunge waliomaliza muda wao kurejea tena kwenye kinyang'anyiro hicho, wateule wa rais kama vile wakuu wa mikoa,wilaya na makatibu wakuu nao pia wamo kwenye mbio hizo.

Kujitokeza kwa wateule hao wa rais ambao sasa uteuzi wao umeshatenguliwa kumezua mjadala mkubwa kuhusu hatma yao ya kisiasa. Baadhi ya watendaji wakuu wa CCM kama katibu mkuu na katibu wake wa uenezi wamekuwa wakionya wateule hao kwa madai ya kiu ya madaraka zaidi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli amesema kuwa jumla ya wagombea wa ubunge waliochukua fomu walifikia 10,367 na waliorejesha fomu hizo kuwa 10,321 na 46 hawakurejesha.

Bernard Membe tansanischer Politiker
Bernard Membe aliyechukua fomu ya kuwania urais kupitia ACT-WazalendoPicha: DW/S. Khamis

Chadema nayo inaendelea na mchakato

Katika hatua nyingine, jumla ya wagombea saba wa chama kikuu cha upinzani chadema wamerejesha fomu za kuwania urais, akiwamo Tundu Lissu, na mwenyekiti wa chama hicho kanda ya kati, Lazaro Nyalandu.

Wanasiasa wengine wanne ambao awali walijotokeza kutangaza kuwania nafasi hiyo kama vile mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa hawakuchukua fomu. Kulingana na mkurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho Reggy Munisi vikao vya chama vinaanza kuketi Jumatatu kutathmini majina ya wagombea hao.

Haijajulikana kama safari hii wapinzani watafanikiwa kuwa na mgombea mmoja au la, na tayari mgombea wa chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe waziri wa zamani wa mambo ya nje, amerejesha fomu za kuwania urais kupitia chama hicho cha upinzani.

George Njogopa, DW Dar es salaam