1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM kutathmini marekebisho ya enzi za Hayati Magufuli

Deo Kaji Makomba
1 Aprili 2022

Mkutano mkuu maalum wa chama kinachotawala nchini Tanzania, CCM, unafanyika jijini Dodoma.

https://p.dw.com/p/49KL9
Tansania Wahlen 2020
Picha: picture-alliance/AP Photo

Pamoja na mambo mengine ajenda kuu itakayotawala mkutano huo ni pamoja na marekebisho yaliyofanywa wakati wa uongozi wa Hayati John Magufuli aliyewaondoa makatibu wakuu wa mikoa kuingia katika vikao vya Halmashauri kuu kwa kile kilichoelezwa kupunguza gharama.

Mkutano mkuu huu maalumu wa CCM umeanza majira ya saa tatu asubuhi ukifunguliwa na mwenyekiti wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, mbele ya wajumbe wake kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Ajenda kuu ya mkutano huo maalumu ilikuwa ni kuliidhinisha jina la kada kindakindaki wa chama hicho Abdulham Kinana lililopitishwa na Kamati  kuu ya CCM na hatimaye kupigiwa kura ya ndio na wajumbe wa mkutano mkuu huo maalumu ambao mbali na ajenda hiyo pia mkutano huo ulifanya marekebisho ya vifungu na kanuni katika katiba yake ikiwa ni pamoja na sehemu ya nane ya marekebisho kwenye ibara ya 91 kifungu kidogo cha kwanza mpaka cha tisa kama anavyoelezea Katibu mkuu wa CCM Daniel Shongolo.

Wajumbe wa chama Chama Cha mapinduzi CCM wakikutana Julai 11, 2020 mjini Dodoma Tanzania.
Wajumbe wa chama Chama Cha mapinduzi CCM wakikutana Julai 11, 2020 mjini Dodoma Tanzania.Picha: imago images/Xinhua

Awali akimuelezea Kinana kabla ya zoezi la kupiga kura mmoja wa wa makada wa chama hicho na aliyewahi kushika nafasi za juu katika awamu mbalimbali kwenye serikali ya chama cha CCM, Steven Wasira alisema kuwa Kinana anazo sifa za kuwa makamu mwenyekiti wa CCM kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya ndani ya serikali na chama kwa ujumla hususani wakati chama hicho kilipopoteza mvuto na kukabiliwa na upinzani mkali kutoka vyama vya siasa mnamo mwaka 2012.

Hadi tunakwenda mitamboni zoezi la kuhesabu kura lilikuwa likiendelea.

Chama cha Mapinduzi  kimekuwa na desturi ya kujitathmini kila baada ya uchaguzi mkuu na baadhi ya wadadisi wa masuala ya siasa wanasema mabadiliko haya ya katiba ni sehemu ya mkakati wa chama hicho kujaribu kuzikabili changamoto za wakati huu.