CAIRO: Jumuiya ya nchi za kiarabu yataka mapigano ya Gaza yakome
4 Oktoba 2006Viongozi wa jumuiya ya nchi za kiarabu wametoa mwito mapigano kati ya Fatah na Hamas katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan yakome mara moja. Wameitaka Marekani ianzishe juhudi mpya za kudumisha amani katika Mashariki ya Kati.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice, akiwa katika ziara yake ya Mashariki ya Kati, amewatolea mwito wapalestina waache kupigana.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Misri, Ahmed Aboul Gheit, amesema baada ya kukutana na Condoleezza Rice, kwamba tatizo la Palestina ni baa la eneo zima la Mashariki ya Kati. Ameongeza kusema la muhimu ni vipi amani itakavyopatikana katika eneo hilo.
Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia, Saud al Faisal, amesema mzozo kati ya Israel na Palestina umelivuruga eneo la Mashariki ya Kati na ameulinganisha na ugonjwa mwilini unaoyakaribisha magonjwa mengine yaushambulie mwili uliodhoofika.