CAF yashikilia uamuzi wake kuhusu Rwanda
1 Septemba 2014Uamuzi huo wa CAF una maana kuwa Kongo Brazzaville itapambana katika Kundi A pamoja na mabingwa watetezi Nigeria, Afrika Kusini na Sudan. Rwanda walitimuliwa kutoka hatua ya kufuzu baada ya kupatikana na hatia ya kumshirikisha mchezaji Dady Birori-Etekiama Agiti Taddy katika awamu ya mechi za mwanzo walizoshinda Libya na Kongo Brazzaville.
Ombi lililowasilishwa na Libya dhidi ya mchezaji huyo halikufaulu, lakini la Kongo likafuzu. Birori hutumia jina la Taddy anapoichezea klabu ya AS Vita nyumbani alikozaliwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Ana vyeti viwili vya uraia wa Rwanda na Kongo pamoja na maelezo tofauti kuhusu tarehe za kuzaliwa ambapo moja inasema ana umri wa miaka 24 na nyingine inasema 28. Boonie Mugabe afisa wa mawasiliano wa SHirikisho la Soka nchini Rwanda, FERWAFA anasema kwa sasa maafisa husika wanashauriana kuhusu uwezekano wa kuwasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya FIFA ya Kusuluhisha Migogoro makao yake nchini Uswisi.
Mwandishi; Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Saumu