BVB kidedea, Bayern hoi
4 Februari 2019Borussia Dortmund ilipanua uongozi wake juu ya msimamo wa ligi kwa pointi moja zaidi hadi pointi saba sasa baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na wenyeji Eintracht Frankfurt mjini Frankfurt. BVB huenda imepoteza pointi mbili muhimu mjini Frankfurt lakini Marco Reus anaendelea kupachika mabao , na goli lake la 13 siku ya Jumamosi lilikuwa na maana huu ni msimu wake mzuri kabisa baada ya michezo 20 ya ligi.
Licha ya kupoteza nafasi kadhaa kuongeza idadi ya mabao yake katika mchezo huo , kama ilivyokuwa wiki moja kabla dhidi ya Hannover 96, Reus yuko njiani kuipiku rekodi yake ya msimu wa 2011/12 alipofunga mabao 18 wakati akicheza katika kikosi cha Borussia Moenchengladbach. Mbinyo kwa mabingwa watetezi Bayern Munich unaongezeka baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Bayer 04 Leverkusen siku ya Jumatatu ambayo ilishuhudia ikiporomoka hadi nafasi ya tatu katika Bundesliga.
Mabingwa hao watetezi wanakabiliwa na mapambano magumu katika wiki hizi mbili wakati katikati ya wiki hii inakabiliana na Hertha Berlin katika kombe la Ujerumani , DFB Pokal ikifuatiwa na mchezo wa duru ya kwanza ya Champions League duru ya mtoano ya timu 16 dhidi ya Liverpool ya Uingereza baadaye mwezi huu.
Kocha Niko Kovac wa Bayern alikuwa hana jibu dhidi ya kikosi cha kocha Peter Bosz wa Leverkusen licha ya kuanza kulifumania lango la wenyeji katika dakika ya 41 ya mchezo.
Gladbach yachupa
Borussia Moenchengladbach ilichupa na kuipita Bayern Munich katika msimamo wa ligi na kuchukua nafasi ya pili kwa wingi wa magoli, timu zote zikiwa na pointi 42 kutokana na michezo 20 ya Bundesliga hadi sasa. Kwa mara ya kwanza katika miaka 33, Gladbach imeweza kushinda michezo mitatu ya mwanzo ya mwaka .
Pia ni pointi zake nyingi kutia kibindoni katika michezo 20 tangu msimu wa mwaka 1969/70 na tena msimu wa mwaka 1976/77 wakati katika misimu yote hiyo iliweza kumaliza kwa kushinda taji la ubingwa wa Bundesliga. Kikosi cha kocha Dieter Hecking cha Gladbach pia ni timu pekee ambayo nyavu zake hazijatikiswa katika Bundesliga tangu kuanza mwaka huu wa 2019.
Kwa upande wa kombe la Ujerumani , timu zitawania kuingia katika duru ya robo finali kuanzia kesho ambapo mabingwa mara nne Borussia Dortmund watakuwa na ndoto ya kupata mataji mawili ya nyumbani kama mwaka 2012 wakati watakapoikabili Werder Bremen katika mchezo wao wa duru ya timu 16 kesho Jumanne.
Dortmund imecheza katika kila fainali tangu mwaka 2011 wakati RB Leipzig ina lenga kuingia katika robo fainali yake ya kwanza wakati watakapokumbana na mabingwa wa mwaka 2015 Wolfsburg siku ya Jumatano.
Pambano lingine la timu za ligi daraja la kwanza katika Bundesliga ni kati ya Schalke 04 dhidi ya Fortuna Dusseldorf, wakati Hamburg SV iliyoko daraja la pili inapambana na Nuremberg ya daraja la kwanza, Heidenheim ina miadi na Bayer 04 Leverkusen na Holstein Kiel inaikaribisha Augsburg, bila kusahau pambano la miamba wa daraja la pili kati ya MSV Duisburg dhidi ya Paderborn.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / ape / dpae
Mhariri: Idd Ssessanga