1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yawakamata maafisa 4 wa kijeshi mauaji ya Ndadaye

26 Novemba 2018

Burundi imewatia nguvuni maafisa wanne wastaafu wa jeshi na kutoa waranti ya kukamatwa rais wa zamani kwa tuhuma za kushiriki mauaji ya rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia, Melchoir Ndadaye, mwaka 1993.

https://p.dw.com/p/38u5C
Bildergalerie 50-jähriges Jubiläum der Afrikanischen Union AU
Picha: DABROWSKI/AFP/Getty Images

Maafisa wanne wastaafu wa jeshi nchini Burundi waliohudunmu kwenye utawala wa Rais Pierre Buyoya wamekamatwa na kupelekwa katika magereza ya mikoani huku ukitolewa waranti pia wa kukamatwa Buyoya na maafisa wengine zaidi ya 10, wote wastaafu jeshini.

Uamuzi huo ulitangazwa siku ya Jumamosi na Mwanasheria Mkuu Sylvestre Nyandwi, ambaye alisema wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya rais wa kwanza kuchaguliwa chini ya misingi ya kidemokrasia nchini Burundi, Melchior Ndadaye.

Mwanasheria mkuu huyo alisema kukamatwa kwao ni katika dhamira ya kukomesha tabia ya  kutowaadhibu wahalifu kama ilivyodaiwa na raia na jamii ya kimataifa.

Katika mahojiano na waandishi wa habari, Nyandwi alisema licha ya kuwa kesi juu ya mauwaji ya Ndadaye ilikuwa tayari mahakamani na hukumu kutangazwa lakini  taasisi yake ilikuwa tayari imeitaka korti kuu isikilize upya kesi hiyo.

"Mahakama Kuu ilitakiwa kubainisha msimamo wake baada ya kudhihirika kuwa kesi hiyo bado haijakamika. Kwani ilitambulika baadaye kuwa kuna watu waliokuwa na jukumu kubwa katika ukatili huo ambao bado hawajafuatiliwa na sheria," alisema Nyandwi.

Waliokwisha kamatwa ni pamoja na Kanali Gabriel Gunungu, Kanali Anicet Nahigombeye, Kanali Niyonkuru na Jemedari Celestin Ndayisaba. Wote wanne ni maafisa waastafu jeshini waliohudumu kwenye utawala wa Buyoya. 

Buyoya naye kukamatwa

Hayo yakijiri, taarifa zinasema hata Buyoya, ambaye ni sasa anauwakilisha Umoja wa Mataifa nchini Mali na katika Ukanda wa Sahel, naye tayari ameshatolewa waranti wa kimataifa wa kutaka akamatwe pamoja na maafisa wengine wa jeshi waliostaafu 18. Miongoni mwa maafisa hao ni pamoja na Kanali Bernard Busokoza aliyewahi kuwa makamu wa rais chini ya utawala wa Rais Pierre Nkurunziza. 

Chama cha Sahwanya Frodebu cha Marehemu Ndadaye, mbali na kukaribisha hatua hiyo, kilisema lazima izingatie mpango mzima wa utangamano kitaifa na kwamba kesi ya watuhumiwa hao walikubaliana kwenye mikataba ya usitishwaji mapigano ishughulikiwe kwenye Tume ya Ukweli na Maridhiano.

Mali-Konferenz in Brüssel
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Mali na Ukanda wa Sahel, Pierre Buyoya (kushoto), anatakiwa pia kukamatwa kwa mujibu wa taarifa kutoka Bujumbura.Picha: picture-alliance/AP Photo

Tume hiyo iliongezwa muda wake wa kazi na kuteuliwa wajumbe wake wapya wiki iliyopita  ambapo sasa inaongozwa na Pierre Claver Ndayicariye, mkuu wa zamani wa Tume ya Uchaguzi (CENI) na Karenga Ramadhani akiwa miongoni mwa wajumbe 15 wa tume hiyo (CVR). 

Familia za maafisa hao wastaafu jeshini waliokamatwa, na ambao wote ni kutoka jamii ya Watutsi, zinasema zinahofia usalama wao ambapo wastaafu hao wanaelemewa na umri mkubwa na baadhi wakikabiliwa na matatizo ya afya. 

Mwandishi: Hamida Issa/DW Bujumbura
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman