1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yatangaza posho kwa wazee

2 Oktoba 2018

Serikali ya Burundi imeamua kugawa faranga 20,000 (dola 11) kwa mwezi kwa kila mzee ili kukabiliana na hali ya umasikini mkubwa kwa wazee ambayo huwafanya baadhi wakiishi kama omba omba mitaani.

https://p.dw.com/p/35qr2
Burundi Wahlen
Picha: Getty Images/AFP

Ndayizeye Riziki anaishi kitongoji cha Buterere kandoni mwa mji mkuu, Bujumbura. Anasema ana umri wa miaka 65 na ni mjane aliyebahatika kupata mtoto mmoja tu katika umri wake.

Bibi huyu, kama walivyo mamia ya wengine wa umri wake, anaishi kwa kupitapita katika mitaa yenye maduka ya katikati ya mji wa Bujumbura akitafuta wa kumsaidia ili apate kunuwa chakula.

Bibi Riziki anasema sasa anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu. Aligunduwa hilo, baada ya kumpata muhisani aliyemlipia matibabu, ambapo vipimo vilionesha kuwa ana ugonjwa huo wa moyo. 

Tayari madaktari wa moyo wamemkataza kula chakula chenye chumvichumvi na mafuta, lakini bimkubwa huyu anasema hana jinsi ya kupata chakula kilicho tafauti na hivyo alivyopigwa marufuku. Na sasa, ugonjwa huo tayari umemdhoofisha na kumfanya kushindwa kupitapita maaduka mengi kuomba msaada. 

Msaada wa serikali

Serikali ya Burundi inasema kuna wazee wengi wanaoishi katika hali duni. Hivyo imeahidi kuchukuwa hatua kadhaa ili kuboresha hali yao ya maisha. 

Waziri wa Burundi anayehusika na haki za binaadamu na mshikamano wa kitaifa, Martin Nivyabandi, anasema miongoni mwa hatua zilizotangazwa mwaka huu ni pamoja na kuwapatia faranga 20,000 (sawa na dola 11 za Kimarekani) "wazee watakaoorodheshwa kuwa masikini zaidi kwenye mikoa yote ya nchi."

Pamoja na msaada huo, anasema Nivyabandi, kutaanzishwa vituo vinavyowahudumiwa wazee sehemu mbalimbali za nchi.

Licha ya hatua hizo, Waziri Nivyabandi anasema bado safari imesalia ndefu, kwani kuna wazee wengi ambao wako katika hali mbaya sana. Lakini "serikali itaendeleza juhudi huku ikihamasisha kuwepo na mshikamano wa kitaifa vijijini katika kuwahudumia na kuwahifadhi wazee."

Hivi karibuni serikali ilianzisha mpango wa kuwaondoa wazee wanaoombaomba mitaani na kuwarejesha katika vijiji vyao vya asili. Lakini ukosefu wa msaada wa kuwawezesha wazee hao kuishi huko vijijini ulisababisha wengi wao kurejea muda mfupi baadaye mjini Bujumbura na katika miji mingine wanakopata msaada kwa kuombaomba mitaani. 

Mwandishi: Hamida Issa - DW Bujumbura
Mhariri: Mohammed Khelef